Habari

CORONA: Hofu yatanda Baringo

March 16th, 2020 1 min read

Na FLORAH KOECH

HOFU imetanda mjini Kabarnet, Kaunti ya Baringo tangu Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa watu watatu wameambukizwa virusi vya corona humu nchini.

Jumatatu, kumekuwa na idadi ndogo ya watu katika vituo vya mabasi.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa wahudumu wa magari ya umma walikuwa na dawa za kuua viini ambapo kila abiria alitakiwa kupitisha mikononi wakati wa kupanda na kushuka.

Madereva pia walinyunyizia dawa ndani ya matatu kabla ya kuruhusu abiria kuabiri.

Wakazi wa Kabarnet, hata hivyo, wameelezea wasiwasi wao kuwa virusi hivyo huenda vikasambaa kwa kasi zaidi humu nchini iwapo serikali haitaongeza juhudi za kukabiliana na maambukizi.

Andrew Kiloo ambaye ni mkazi wa Kabarnet,  alisema kuwa tangazo la serikali la Jumapili kuhusina na uwepo wa virusi vya corona humu nchini huenda likasababisha watu kukosa chakula.

“Wengi wetu tunafanya kazi ya kibarua. Tunapata riziki yetu baada ya kufanya kazi. Tukikosa kwenda basi hatutapata chakula na huenda tukafa,” akasema Bw Kiloo.

Wakazi hao pia waliitaka serikali kuwapa dawa za kuua viini bila malipo huku wakisema kuwa wengi wao hawawezi kumudu.

“Idadi kubwa ya Wakenya hawawezi kumudu kula mara tatu kwa siku na hivyo ni vigumu kwao kununua dawa ya kuua viini,” akasema Bw Kiloo.

Afisi nyingi za serikali katika mjini Kabarnet, kikiwemo kituo cha Huduma, jana zilifungwa.

Rais Kenyatta Jumapili alithibitisha kuwa watu wawili zaidi walipatikana na virusi vinavyosababisha homa ya corona. Idadi ya watu walio na virusi hivyo imefikia watatu.

Rais Kenyatta alisema waathiriwa wawili hao walibainika baada ya kupima watu 27 walioshukiwa kutangamana na mwathiriwa wa kwanza.