Habari

CORONA: Huenda serikali ikafunga jiji la Nairobi

April 3rd, 2020 2 min read

Na JUMA NAMLOLA

SERIKALI Alhamisi ilitoa ishara kuwa huenda ikalazimika kufunga shughuli zote katika kaunti ya Nairobi, kama njia ya mwisho ya kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Kwenye hotuba yake ya kila siku, Waziri wa Afya Bw Mutahi Kagwe, aliwataka waakazi wa Nairobi waanze kuzoea kutotoka nje, kwa kukaa kwenye makazi yao.

“Nataka nikariri kwamba tunaendelea kuonya watu wasiwe na vijisafari vya mara kwa mara, hasa kutoka Nairobi kwenye mashambani. Hatari ya jambo hili iko wazi. Ni rahisi sana kusambaza virusi vya corona kwa wanaoishi mashambani, hasa wakongwe, kama ilivyofanyika nchini Italia,” akasema Bw Kagwe.

Waziri alieleza kuwa hakuna haja kwa watu kuondoka Nairobi na kuwatembelea watu msimu wa Pasaka.

“Si lazima uende mashambani ndipo Pasaka yako ikamilike. Tunapendekeza kuwa kusiwe na misafara yoyote kutoka au kuingia Nairobi, isipokuwa magari ya kubeba vyakula pekee. Na nyinyi watu wa nje ya Nairobi, kama unaishi Nyeri, Kisumu au kaunti nyingine yoyote, kaa huko uliko. Si lazima uende Nairobi,” akasema.

Huenda hatua hiyo ya serikali inatokana na takwimu zinazoonyesha kuwa, idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya corona ni wa kaunti ya Nairobi. Kabla ya kuacha kueleza wagonjwa kutokana na wanakotoka, Nairobi ilikuwa ikiongoza kwa watu 37.

Kauli yake ilijiri huku akitangaza kuwa watu wawili waliokuwa katika hali mbaya jana walifariki kutokana na corona. Wawili hao walikuwa katika hospitali za miji ya Nairobi na Mombasa.

Vifo vya wawili hao sasa vinafikisha idadi ya waliouawa na corona nchini kuwa watatu, na walioambukizwa sasa ni 110.

“Katika saa 24 zilizopita, tulifanikiwa kuwapima watu 625 ambapo 29 wamegunduliwa kuwa wameambukizwa. Kati ya hawa, 28 ni Wakenya na mmoja ni raia wa Congo. Hii sasa inafanya idadi ya watu wote walioambukizwa hapa nchini kuwa watu 110,” akasema.

Wagonjwa hao ni wanaume 13 na wanawake 16 walio na umri wa kati ya miaka 15 na 64.

Waziri aliwataka Wakenya wasidanganywe na watu wachache wanaodhani kuwa corona ni maradhi ya kufikirika, na kuwataka wajilinde sasa kabla hawajachelewa.

“Wakenya wenzangu, sitaki kuwatisha lakini takwimu hizi zinaonyesha kuwa maradhi haya yanaendelea kuzagaa. Usitake kuuliza ni kwa nini hujaona mtu unayemjua akiwa ameuawa na maradhi haya. Wakati ukiona mtu huyo, utakuwa umechelewa sana,” akasema.

Virusi vya corona kinyume na maradhi mengine, havisambai vyenyewe.

Ili kusaidia katika juhudi za kupambana na maradhi hayo, waziri alisema serikali inapanga kuajiri wafanyikazi wa afya 5,000 kufikia Jumatano ijayo.

“Tumewaagiza Makamishna wa Kaunti na walimu wakuu wa shule za bweni kote nchini, waanze kutathmini uwezekano wa taasisi hizo kutumika kuwahifadhi wagonjwa,” akasema.