Habari Mseto

CORONA: Idadi ya maambukizi yapanda tena huku Wizara ya Afya ikionya dhidi ya mikutano ya hadhara

October 9th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WIZARA ya Afya imewaonya Wakenya dhidi ya kuhudhuria mikutano ya kisiasa na ile ya kijamii ili kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman ametoa onyo hilo Ijumaa wakati akitoa takwimu zinazoonyesha kuwa visa 442 vipya vya maambukizi ya virusi hivyo vimenakiliwa nchini ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.

“Kwa mara nyingine tunawaonya raia dhidi ya kukongamana katika mikutano ya kisiasa na kijamii ili wasijiweke katika hatari ya kuambukizwa virusi vya corona. Waendelee kuzingatia masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya,” akasema.

Wanasiasa wa mirengo ya ‘Kieleweke’ na ‘Tangatanga’ na wale wa vyama vya upinzani wamekuwa mbioni wakichapa kampeni za kujitafutia umaarufu kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Dkt Aman amesema visa hivyo vipya viligunduliwa baada ya sampuli kutoka kwa jumla ya watu 5,327 kufanyiwa uchunguzi.

Idadi hiyo sasa inafikisha 40,620 idadi jumla ya maambukizi nchini tangu kisa cha kwanza cha Covid-19 kilipogunduliwa nchini.

Kwa mara ya kwanza, Kaunti ya Nakuru inaongoza kwa visa vipya kwa kuandikisha visa 94 ikifuatwa na Nairobi yenye visa 80.

Mombasa ni ya tatu kwa visa 47, Uasin Gishu (22); Embu na Kisumu (visa 20 kila moja); Turkana (18); Meru (15); Trans Nzoia (14); Kisii (13); Garissa na Kilifi (visa 12 kila moja); Siaya na Kajiado (visa 11 kila moja); Baringo, Kiambu na Kericho (visa 10 kila moja); Taita Taveta (4); Kwale, Migori, Machakos, Nandi na Vihiga (visa 2 kila moja).

Kaunti za Bugoma, Elgeyo Marakwet, West Pokot, Nyandarua, Kitui, Kirinyaga, Murang’a, Kakamega na Bomet zimenakili kisa kimoja kila moja.

Idadi ya wagonjwa waliofariki kutokana na Covid-19 imepanda hadi 755 baada ya wagonjwa nne zaidi kuthibitishwa kufariki ndani ya saa 24 zilizopita.

“Habari nzuri ni kwamba wagonjwa 166 wamepona na kuruhusiwa kuondoka hospitalini. Idadi hiyo inafikisha 30,876, idadi jumla ya wale ambao wamepona,” akasema Dkt Aman.