Habari

'Corona ilifanya Raila kurejea nchini bila mbwembwe'

July 14th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

UONGOZI wa ODM umesema kiongozi wake Raila Odinga alirejea nchini kimyakimya ili kuzuia kuvutia umati mkubwa wa wafuasi wake na hivyo kuepuka hali ya ukiukaji wa masharti ya serikali ya kudhibiti maambukizi ya Covid-19.

Mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho John Mbadi alisema urejeo wa Bw Odinga haukutangazwa waziwazi ili wafuasi wake wasifurike katika uwanja wa ndege wa JKIA, Nairobi kumkaribisha.

“Hatukutaka kutangaza kuwa Raila anarejea kwani umati mkubwa ungekusanyika katika uwanja wa ndege kumkaribisha nyumbani. Hatukutana watu wengi wafike uwanja wa ndege kusudi tusionekane kuvunja kanuni ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Hii ndio maana tumehakikisha amerejea bila mbwembwe nyingi,” akasema mbunge huyo ambaye ni kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa.

“Bw Odinga ni kiongozi ambaye amekua akiwahimzia watu kutotangama na hivyo hangechangia uwepo wa mazingira ambapo watu wanakiuka sharti hili,” akaongeza Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini.

Mwenyekiti huyo wa ODM alisema Bw Odinga atakuwa akiendesha shughuli zake nyumbani kwake Karen, Nairobi kwa kipindi cha majuma mawili yajayo na ni wageni wachache pekee wataruhusiwa kumwona.

“Hata hivyo yu’ buheri wa afya. Hawezi kurejea afisini mwake wakati kwa sababu watu wengi watataka kufika huko kila siku kumjulia hali. Matokeo yake ni kwamba umati wa watu utakuwepo hapo kila mara kinyume na kanuni za Covid-19,” akasema Bw Mbadi.

Katika hali ya kawaida, Bw Odinga ambaye pia ni mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika (AU) huendesha shughuli zake rasmi katika afisi zake zilizoko jumba la Capitol Hill, katika mtaa wa Upper Hill.

Bw Odinga alirejea nchini mwendo wa saa nne usiku Jumapili kutoka Dubai ambako amekaa kwa majuma matatu akipokea matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji. Aliwasili kwa ndege ya kifahari ya kukodishwa.

Mnamo Julai 1, 2020, kiongozi huyo wa ODM aliwashukuru Wakenya waliotumia jumbe za heri njema wakati ambapo alikuwa akipokea matibabu katika jijini Dubai.

Katika video iliyosambazwa na bintiye, Winnie, Bw Odinga ambaye alikuwa amevalia fulani manjano na suruali fupi ya rangi ya samawati na vyatu vyeusi, alisema jumbe hizo kutoka kwa Wakenya zilimfanya kupona haraka.

“Nawashukuru marafiki wangu wote, wafuasi na vijana wetu ambao walinutumia jumbe nyingi za heri njema. Hii imenipa moyo zaidi na hata kupona kwa haraka,” akasema.