Corona ilipunguza kasi ya mbinu za kisasa za upangaji uzazi, asema Dkt Aman

Corona ilipunguza kasi ya mbinu za kisasa za upangaji uzazi, asema Dkt Aman

Na CHARLES WASONGA

UTUMIZI wa mbinu za kisasa za upangaji uzazi ulipungua kwa kiwango kikubwa katika Mwaka wa Kifedha wa 2020/2021 kutokana na mlipuko wa janga la Covid-19.

Waziri Msaidizi wa Afya Rashid Aman, Jumapili alisema hii ni licha ya kwamba matumizi ya mbinu hizo za upangaji uzazi miongoni mwa wanawake walioko katika ndoa yalipanda nchini kutoka kiwango cha asilimia 36 mnamo 2007 hadi asilimia 61 mwaka huu.

“Lengo la serikali na Wizara ya Afya lilikuwa kwamba matumizi ya mbinu hizi za upangaji uzazi yafikie kiwango cha zaidi ya asilimia 80 mwaka huu 2021. Lakini lengo hili halikuweza kutimia kwa sababu ya mlipuko wa Covid-19 uliovuruga maisha na kuchangia idadi kubwa ya wanawake kutokwenda katika vituo vya afya kwa huduma hii kwa hofu ya kuambukizwa,” Dkt Aman akasema.

Waziri huyo msaidizi alieleza kuwa licha ya hayo, Kaunti ya Kirinyaga inaongoza kwa utumizi wa mbinu hizo za upangaji uzazi kwa kiandikisha kiwango cha utumizi cha asilimia 77.

“Kwa upande mwingine kaunti za Kaskazini Mashariki mwa Kenya kama vile Mandera zilinakili kiwango cha asilimia 30 cha utumizi wa mbinu za upangaji uzazi. Hii ni kwa sababu wanawake wengi katika maeneo hayo huwa hawapati huduma hizi kwa urahisi,” akaeleza Dkt Aman huku akirejelea ripoti kuhusu Takwimu za Kiafya Nchini (Kenya Demographic Health Survey).

Dkt Aman alisema hayo katika hoteli ya Serena, Nairobi alipoongoza hafla ya mwaka huu katika Maadhimisho ya Matumizi ya Mbinu za Upangaji Uzazi Duniani (World Contraception Day, 2021).

Waziri huyo msaidizi alisema serikali kupitia wizara hiyo imeweka mikakati ya kuimarisha matumizi ya mbinu za upangaji uzazi kama njia ya kuimarisha afya na uchumi wa nchini.

“Serikali inafanya hivyo kwa kuongeza mgao wa fedha kwa Wizara ya Afya na haswa kitengo cha upangaji uzazi na afya ya uzazi. Kwa mfano, katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022 bajeti ya Wizara ya Afya iliongezwa hadi Sh121.1 bilioni kutoka Sh111.7 bilioni katika mwaka wa 2020/2021,” akasema Dkt Aman.

Alisema kiasi kikubwa cha pesa hizo zitaelekezwa kufadhili mpango wa Afya Kwa Wote (UHC) “unaojumuisha huduma za upangaji uzazi”.

“Hata hivyo, kitengo hiki cha upangaji uzazi kingali kinakabiliwa na uhaba wa ufadhili; pengo ambalo huzibwa na ufadhili kutoka mashiriki fadhili,” Dkt Aman akaeleza.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kitaifa Kuhusu Idadi ya Watu na Maendeleo (NCPD) Mohamed Sheikh alitoa wito kwa serikali na mashirika fadhili kuongeza ufadhili kwa sekta ya upangaji uzazi.

“Kando na kuwa suala la kiafya, upangaji uzazi pia ni na suala la maedeleo na hivyo linahitaji ufadhili wa kutosha,” akasema.

Kwa upande wake, Waziri wa Afya katika Kaunti ya Murang’a Joseph Mbai alieleza changamoto ambazo wanawake katika baadhi ya kaunti hupitia wakitafuta huduma za upangaji uzazi.

“Kaunti nyingi bado hazina uwezo wa kununua vifaa vya upangaji uzazi kutokana na changamoto za kifedha. Kaunti zinazoathirika zaidi ni zile zinazopatikana katika maeneo kame (ASAL) nchini,” Dkt Mbai ambaye pia ndiye mwenyekiti wa muungano wa mawaziri wa afya katika kaunti zote 47, akasema.

Waziri wa Afya Kaunti ya Murang’a Dkt Joseph Mbai akihutubu katika hafla hiyo. Picha/ Charles Wasonga

You can share this post!

Olunga afunga mabao 5 kuisaidia Al Duhail kuzamisha Al...

Limbukeni Brentford wawakaba Liverpool koo ligini