Makala

Corona ilivyobadilisha mila za Wabukusu

April 26th, 2020 3 min read

NA HOSEA NAMACHANJA 

Kabila la Wabukusu ni mojawapo ya makabila ya jamii ya Waluhya inayopatikana magharibi mwa Kenya. Kabila hili ndilo lenye watu wengi na linategemea ukulima wa mahindi.

Chimbuko la tohara ya Wabukusu ni jamii ya Wakalenjin. Wabukusu walikopa utamaduni huu karne ya kumi na nane kutokana na utangamano wa mara kwa mara na kabila la Wasabaoti la jamii ya Wakalenjin kupitia kwa shughuli kama vile za biashara,uporaji wa mifugo na ndoa.

Tohara katika kabila la Wabukusu hufanywa kwa watoto wa kiume kati ya miaka kumi na miwili na kumi na minne kwa njia ya kitamaduni kwa kuongozwa na wazee weledi wa utamaduni huu.

Kama sherehe, hufanywa kimsimu ambapo kila msimu huchukua miaka kumi kwa kila karne isipokuwa msimu uitwao msimu wa Bachuma ambao kwa kila karne huchukua miaka kumi na minne.

Hili lilitokana na uwepo wa mzee mmoja wa msimu wa Basawa kutoka kwa msimu wa awali aliyekuwa hai na kimila,hakupaswa kuwa hai wakati huo na baadaye alifariki mwaka wa 1884.

Kwa sababu ya hilo,wazee watamaduni waliamua kwamba,mzee yeyote atakayeishi sana hadi kuonekana kwa msimu mwingine mara ya pili sawa na ule aliopashwa tohara,atauawa.

Fauka ya hayo, wakati wa vita vya pili vya dunia (1939-1945),kabila hili la Wabukusu halikuwapasha watoto wao wa kiume tohara kama ilivyo ada.

Vita vilifanya sherehe ya jando kusitishwa hadi 1948.Kusitishwa kwa sherehe hii kuliamuliwa na kikao cha wazee waliolinda utamaduni huu wakati huo.

Kwa kauli moja, waliamua na kuelewana kuwa,vita vikitokea hasa vinavyoathiri dunia nzima mwaka wa sherehe mwezi wa Agosti,sherehe hii itasitishwa.

“Mwaka wa 1982 nchini, palikuwapo na jaribio la kupindua serikali ya Rais Moi mwezi wa Agosti.Hofu ilitanda katika jamii yetu huku tetesi zikiwa kwamba, sherehe yetu ya kutengeneza vijana ingesitishwa lakini tuliendelea na shughuli yetu” asema mzee Wanyama mmoja wa mangariba kutoka Kaunti ndogo ya Kabuchai, Wadi ya Mukuyuni kwa mahojiano.Hii ni kumaanisha kwamba jaribio lililotokea lilikuwa la hapa nchini na halikuhusisha dunia nzima hivyo sherehe hii iliendelea kama kawaida.

Mwaka huu wa 2020, kuna ugonjwa wa corona ambao unaathiri dunia nzima kama awali vita vya dunia.Nchi nyingi duniani zinapambana nao kutafuta tiba na kuzuia maenezi yake kama vile kuepuka mikusanyiko ya watu,kuvaa barakoa,kutakasa mikono kwa kutumia vieuzi miongoni mwa njia nyingine nyingi.

Nchi yetu ya Kenya nayo kando na kuwahimiza wananchi wake kutumia barakoa, vitakasa mikono pamoja na kuepuka mikusanyiko, shughuli za usafiri katika baadhi ya miji mikuu kama vile Nairobi zimesitishwa na kafyu kwa upande wake kutawala kote watu wakiwa karantini.

Amri hizi za kuzuia maenezi ya maambukizi ya virusi vya korona zinazidi kuwatia tumbo joto Wabukusu na kuwanyima lepe la usingizi.

Wengi waliokuwa wamejiandaa kwa sherehe ya Agosti ya jando mwaka huu kuwapasha wanao tohara kitamaduni,sasa wamebaki vinywa wazi wasijue la ziada.Hawafahamu sherehe hii itasitishwa hadi msimu ujao 2022 au watasherehekea kama ada mwaka huu.

Sherehe hii ambayo imelindwa na katiba chini ya utamaduni,huwa inahudhuriwa na watu wengi mahali wazi hadi baadhi ya Wabukusu walio nje ya Kenya au ndani ya nchi kikazi japo mbali na nyumbani,huomba likizo fupi ili waje waburudike na wenzao ila swali ni je,msimu huu sherehe hii itafanyika?

Je,watatangamana kwa kuimba nyimbo za nyiso na kucheza kama awali? Je,watakesha usiku wakila,wakinywa pombe ya kitamaduni na sarakasi zingine kama awali? Ikumbukwe, serikali imeweka amri ya kutotoka nje usiku (kafyu),watu kuvaa barakoa (maski)na pia imekataa mikusanyiko ya watu.

Hapa,raha ya kufurahia sherehe ya jando imedhibitiwa kila kona kwani,hakuna kukusanyika na kutembea usiku.

Kwa sababu sherehe hii huongozwa na wazee weledi wa utamaduni,wazee hao hadi sasa hawajaongea kitu kwani kulingana na kaida za sherehe,uamuzi huwa haufanywi upesi.

Hii ni ishara tosha kwamba,wazee wamesubiri hadi mwezi wa saba mwishoni ndipo wajue la kufanya.Iwapo ugonjwa huu utakuwepo na tisho kama wakati huu,basi ,Wabukusu hawatakuwa na budi kusitisha sherehe hii.

Wale wataathirika itawabidi wavumilie kwa sababu,ujio wa utamaduni wa wakoloni nchini kwa asilimia kubwa uliathiri utamaduni wa Waafrika.

Hii ina maana kuwa,wapo ambao hufuata utamaduni wa wakoloni kuwapeleka wanao hospitalini kuwapasha tohara na wale walioshikilia,wanashikilia na watazidi kushikilia utamaduni wa kiafrika katu chambilecho mwacha mila ni mtumwa.