Habari Mseto

Corona ilivyochelewesha ndoto za wanafunzi

September 28th, 2020 2 min read

Na ANGELINA MWAKOI

Loice Chanya ni mwanafunzi wa Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Senior Chief Mwangeka Girls High School, katika Kaunti ya Taita Taveta.

Tangu corona ilipoanza kulemaza sekta ya elimu nchini kutokana na kufungwa kwa shule, anasema masomo yake yamerudi nyuma na kuchelewesha ndoto yake.

Yeye ni miongoni mwa wanafunzi wengi ambao wamekata tamaa ya kujiendeleza kimasomo. “Corona imerudisha masomo yangu nyuma sana, nilikuwa nifanye mtihani wangu wa mwisho wa KCSE mwaka huu na kwa sababu ya Covid-19 hilo halitawezekana tena labda mwaka ujao,” aliambia Taifa Leo Dijitali.

Loice, ambaye azma yake maishani ni kuwa daktari baada ya kujiunga na chuo kikuu, amekosa mwelekeo katika kipindi cha miezi sita iliyopita tena. Hata hivyo, bado ana matumaini kwamba shule zitakapofunguliwa ataweza kurejelea ndoto yake.

“Ningependa sana nije kuwa daktari niweze kuwatibu wagonjwa nikimaliza chuo kikuu na nitajitahidi niweze kutimiza lengo langu,” anasema.

Johnson Mwakina, ambaye ni mwanafunzi wa ualimu wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Pwani, anafichua kuwa mwaka huu ulikuwa muhimu sana kwake kwani alitarajia kutumwa katika mojawapo ya shule za upili eneo la Pwani kujifunza kusomesha.

Kwa sasa anahofia kuwa watakaporudi chuoni huenda asipate nafasi hiyo ya kunoa makali ya taaluma yake.

“Nilikuwa niende kujifunza zaidi kwa kuingia darasani na kufundisha wanafunzi, lakini kwa sasa hilo haliwezekani kwa sababu shule za upili zilifungwa na pia vyuo vikuu na kwa sasa tupo nyumbani,” alisema Mwakina.

Anaongeza kuwa imekuwa vigumu kwake kulipia ada ya mtandao ili kushiriki masomo kwa njia ya intaneti, hali inayomeletea wasiwasi kuwa wenzake wanasonga mbele huku yeye akiachwa nyuma.

“Chuo chetu kilianzisha mfumo wa kusoma kwa njia ya mtandao ambayo unahitajika kuwa na shilingi mia moja za kununua vifushi vya data kila siku ndipo uweze kusoma kupitia mfumo huo. Hili limenipa changamoto kwa sababu sina uwezo wa kupata Sh100 kila siku na pia sina kazi yoyote, nategemea wazazi wangu,” alieleza Mwakina.

Hali hiyo ya wanafunzi kusalia nyumbani imewaletea wazazi wengi msongo wa mawazo wasijue ni vipi watawasaidia wana wao.

Kuna wasiwasi mitaani kuwa huenda wanafunzi wakatumia muda vibaya na kujipata katika vikundi hatari vya biashara ya dawa za kulevya.

Kulingana na Ancila Kandi ambaye ni mzazi, wanafunzi wameanza kuiba hela za wazazi wao na kujitosa kwa ulevi.

“Nimewaona wanafunzi wa kidato cha nne wakijiingiza kwa ulevi. Wanaiba pesa za mama zao na kutoweka mchana kutwa kisha kujerea nyumbani usiku wakiwa walevi chakari,” anafichua.

Angela Mwakoi ni mwanafunzi wa uanahabari katika Chuo Kikuu cha Masinde Muliro.