Habari MsetoSiasa

Corona ilivyozika malumbano ya BBI

April 10th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Mpango wa Maridhiano (BBI) ambao kabla ya visa corona kuripotiwa nchini ulikuwa umeshika kasi na kugawanya wanasiasa, huenda ukasahaulika hata baada ya wimbi la virusi hivi kupita.

Tayari serikali inaelekeza nguvu na rasilmali zikiwemo zilizotengewa BBI kupigana na corona na mwenyekiti wa Jopokazi hilo, Yusuf Haji ametangaza kuwa haliwezi kukutana kwa sababu ya corona.

“ Hatuwezi kuendelea na shughuli zetu hadi serikali itakapotangaza agizo la watu kukutana,” Bw Haji alisema.

Kamati ya Haji ilikuwa imekamilisha kukusanya maoni kutoka kwa umma na ilikuwa katika harakati za kuandika ripoti ambayo ingewasilisha kwa Rais Kenyatta.

Muda wa kuhudumu wa kamati hiyo unakamilika Juni mwaka huu wakati ambao wataalamu na wizara ya afya wanasema Kenya itakuwa bado ikikabiliana na maambukizi ya corona.

Kwenye hotuba yake ya kila siku kuhusu corona, waziri wa Afya Mutahi Kagwe amekuwa wakionya kuwa itachukua muda kufaulu kuzua maambukizi ya corona.

“ Itachukua miezi mitatu au minne, hatuwezi kufaulu mara moja,” Bw Kagwe alisema Jumanne akitaja corona kama suala ambalo serikali inapatia kipaumbele kwa wakati huu.

Wadadisi wanasema kulingana na hali ilivyo, corona itazika BBI katika kaburi la sahau.

“ Mambo mengi yamesitishwa ili nguvu zote na rasilmali zielekezwe kukabiliana na corona na wimbi litakapopita, hali itakuwa imebadilika na uchumi kuwa katika hali mbaya. Serikali itakuwa ikipambana kufufua uchumi na sio BBI,” asema mdadisi wa siasa Nicholas Mutungi.

Waziri wa Fedha, Ukur Yatani ametangaza kuwa corona itaathiri ukuaji wa uchumi wa Kenya.

“ Utakuwa ukosefu wa uwajibikaji kwa serikali kupatia kipaumbele BBI baada ya wimbi la corona badala ya kusaidia Wakenya kupata nafasi za kazi kwa kufufua kampuni na biashara ambazo zimeathiriwa na janga hili,” asema.

Rais Uhuru Kenyatta na mshirika wake katika handisheki, Raila Odinga walikubaliana kutumia Sh11 bilioni zilizokuwa zimetengewa BBI kukabiliana na maambukizi ya corona.

Mikutano ya uhamisho ya BBI ilikuwa imegawanya Wakenya walioiunga wakitaka kura ya maamuzi kubadilisha katiba na walioipinga wakiwalaumu mchakato huo kama njama ya watu wachache wanaotaka kubuni nyadhifa wajiunge na serikali.

Wadadisi wanasema itachukua muda kufufua mjadala kuhusu BBI.

“Baada ya wimbi la corona, kwa serikali inayowajibika, itachukua muda kurejesha mjadala wa BBI. Na hata kama utarejeshwa, mazingira yatakuwa yamebadilika pakubwa,” asema.

Hatua ya kuhamisha pesa zilizotengewa BBI kukabiliana na maambukizi ya corona, tamko la Bw Haji ni pigo kwa waliokuwa wakitaka kura ya maamuzi kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Bw Odinga aliyekuwa akiongoza mikutano ya uhamisho ya BBI katika maeneo tofauti amekoma kuzungumzia suala hilo na amekuwa wakiwahimiza Wakenya kufuata maagizo ya serikali ya kukabiliana na maambukizi ya corona.

Naye Rais Kenyatta ambaye alikuwa akiunga mchakato huo akisema ulilenga kuunganisha Wakenya amesema atafanya kila awezalo kulinda Wakenya na janga la corona