Corona imeathiri uwezo wa wanaume kuzalisha – Utafiti

Corona imeathiri uwezo wa wanaume kuzalisha – Utafiti

Na MASHIRIKA

UTAFITI mpya umeonyesha kuwa Covid-19 inaweza kufanya wanaume kukosa uwezo wa kuzalisha.Wanasayansi wanasema kwamba wanaume wanaoambukizwa virusi hivyo wanaweza kukosa kuzalisha kwa muda.

Kwenye utafiti wao wanasayansi walilinganisha ubora wa shahawa za wanaume walioambukizwa na wasioambukizwa virusi hivyo na wakafikia uamuzi kwamba vinaathiri uwezo wa mwanamume wa kuzalisha.

Kufuatia utafiti huo, wanasayansi wanashauri wanaume waliopona corona kuchunguzwa afya yao ya uzazi kabla ya kujaribu kuzalisha lakini wakaonya kwamba utafiti wao sio mkamilifu.

Wanasayansi walilinganisha wanaume 105 ambao hawakuwa na virusi hivyo na 84 waliothibitishwa kuwa navyo na kupima shahawa zao kwa siku kumi ndani ya muda wa siku 60.

Waligundua kwamba shahawa za wanaume walioambukizwa corona zilikuwa dhaifu kuliko za wale ambao hawakuwa wameambukizwa.Idadi, kiwango na umbo la shahawa za wanaume walioambukizwa corona pia ziliathiriwa vibaya na virusi hivyo.

Kulingana na watafiti hao, athari ziliongezeka kulingana na jinsi mwanamume alivyoathiriwa na virusi hivyo.

“Athari katika shahawa kunahusishwa na kiwango cha chini cha ubora wa shahawa na upungufu wa uwezo wa kuzalisha. Ingawa athari hizi zilionekana kuondoka baada ya muda, zilibaki kuwa za juu katika wagonjwa wa COVID-19 na kiwango cha mabadiliko kilitegemea jinsi ugonjwa huo ulivyoathiri mtu,” alisema kiongozi wa utafiti huo Behzad Hajizadeh Maleki, wa chuo kikuu cha Justus Liebig Giessen, Hesse, Ujerumani.

Hata hivyo, wataalamu ambao hawakushiriki katika utafiti huo walitilia shaka ripoti hiyo na kuonya hayafai kuchukuliwa kama hali halisi ilivyo.

“Ninataka kutoa onyo kuhusu fasiri yao. Kwa mfano, wanasema kwamba maambukizi ya corona yanasababisha uharibifu katika mfumo wa uzazi wa mwanamume ilhali kinachoonekana katika utafiti wao ni uhusiano tu,” Profesa Allan Pacey, wa The University of Sheffield, South Yorkshire, Uingereza aliambia CNN.

Baada ya kuchunguza tafiti 14 zilizochapishwa kuhusu mada hiyo, Pacey alisema alifikia uamuzi kwamba athari zozote za corona kwa uwezo wa kuzalishwa kwa mwanamume ni ndogo na za muda mfupi.

Asema matokeo ya utafiti huo yanaweza kuchangiwa na mambo mengine kama vile matumizi ya dawa za kutibu virusi hivyo jambo ambalo watafiti walikiri katika ripoti yao.

“Kuambukizwa virusi vyovyote kama vya homa kunaweza kupunguza idadi ya shahawa kwa wiki chake au miezi. Hii inafanya vigumu kuamua kiwango cha upungufu kilichogunduliwa katika kwenye utafiti kilihusishwa na COVID-19,” alisema Dkt. Channa Jayasena wa Imperial College London.

“Ni muhimu kufahamu kwamba hakuna ushahidi kwamba virusi vya corona vinapatikana katika shahawa za mwanamume na hakuna ushahidi kwamba virusi hivyo vinaweza kusambazwa kupitia shahawa,” akasema Alison Murdoch, anayesimamia Newcastle Fertility Centre katika chuo kikuu cha Newcastle, Uingereza.

You can share this post!

TAHARIRI: Tusiwe na pupa ya kurudisha kiboko

Ruto alia ‘mahasla’ wanamfyonza