Habari

Corona imeisha Tanzania – Magufuli

June 8th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

HUKU ulimwengu, hasa mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki, ukiendelea kupambana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona, Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, ametangaza kuwa nchi hiyo imefanikiwa kuangamiza kabisa janga hilo.

Akizungumza Jumapili katika Kanisa Katoliki la Parokia ya Bikira Maria Imakulata mkoani Dodoma, Dkt Magufuli alisisitiza kuwa ugonjwa huo umetokomea nchini humo kwa sababu ya maombi.

“Mimi ninaamini na nina uhakika Watanzaina wengi wanaamini ugonjwa wa corona umeondolewa kwa nguvu za Mwenyezi Mungu katika nchi yetu. Ninamshukuru sana Mungu wetu. Watanzania wanampenda Mungu na ndiyo maana hata corona ‘imekoromea’ huko mbali,” akasema.

Hata hivyo, aliwataka Watanzania waendelee kujikinga kwa njia za kiasili kama vile kujifukizia dawa za miti-shamba.

Alitilia mkazo pia msimamo wa Wizara ya Afya nchini humo kwamba wagonjwa wanne pekee ndio wamelazwa hospitalini kitaifa wakiugua ugonjwa huo.

“Corona imeisha. Nilikuwa ninapata habari kutoka kwa Waziri wa Afya majuzi, ambapo aliniambia kwamba Dar es Salaam kulikuwa na watu wanne pekee walioambukizwa virusi. Najua kutakuwa na uzushi mwingi utakaotolewa, lakini lazima tujifunze kumtanguliza Mwenyezi Mungu,” alisema hayo kwa wajumbe waliohudhuria mkutano wa kila mwaka wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (TTU) jijini Dodoma mnamo Jumamosi.

Kwenye mkutano huo, kadhalika, Rais Magufuli alipiga marufuku uvaaji wa barakoa hasa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

Alisema kuna uwezekano barakoa zinazosambazwa zina virusi vya corona na hivyo ni hatari kwa wananchi wanaozitegemea.

Kwenye hotuba yake iliyopeperushwa moja kwa moja, Rais Magufuli aliwaonya watu na taasisi zinazosambaza vifaa vya kujilinda dhidi ya maambukizi hayo, ambavyo havijaidhinishwa na mamlaka husika.

Kwenye mkutano huo uliofanyika katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, wajumbe hao waliketi kwa kukaribiana huku wakikosa kuvaa barakoa. Magufuli aliwasifu kwa hilo.

Serikali ya Tanzania imesema kuwa inatathmini uwezekano wa kufungua upya shule za msingi na upili kutokana na kupungua kwa maambukizi ya viriusi vya corona nchini humo.

“Kutokana na kuendelea kupungua kwa visa vya maambukizi ya corona kadri siku zinavyosonga, ninatathmini uwezekano wa kufungua upya shule za msingi na upili. Tutavishinda virusi hivi kupitia maombi na kuzingatia maagizo yanayotolewa na wataalamu wa afya,” akasema.

Pendekezo hilo la serikali linajiri baada ya kufungua vyuo anuwai, vyuo vikuu na kidato cha sita.

Tanzania imekuwa ikitangaza hatua zinazogutusha ulimwengu katika harakati ya kukabiliana na corona.

Mbali na kupiga marufuku barakoa, Rais Magufuli amewahi kukashifu vifaa vya kupima uwepo wa virusi hivyo baada ya kudai kuwa sampuli za kondoo na papai zilipatikana kuwa na ugonjwa huo.

Kufikia sasa, hali halisi ya ueneaji wa virusi vya corona nchini humo imebaki kuwa siri kubwa ya serikali kwani iliacha kutangaza takwimu zake.

Rais Magufuli aliendelea kusisitiza kuwa maambukizi ya ugonjwa huo si jambo kubwa, na taifa lake linaweza kushinda Covid-19 kwa maombi.