‘Corona imenisukuma kwa kona’

‘Corona imenisukuma kwa kona’

Na SAMMY WAWERU

DICKSON Muceri amekuwa mkazi wa Nairobi kwa muda wa miaka kadhaa ila sasa kitovu hicho cha jiji kuu la nchi hakikaliki tena.

Mwaka uliopita, Kenya ilipokumbwa na virusi vya corona, aliathirika kwa kiasi kikubwa.

Muceri, 38, alikuwa mmiliki wa tuktuk mtaani Githurai, kiungani mwa jiji la Nairobi, biashara ambayo aliingilia kitambo ili kujiendeleza kimaisha.

Hata ingawa amejaribu biashara zingine, anasema huduma za tuktuk zina mapato.

Baada ya Machi 2020, sheria na mikakati kuzuia maenezi ya Covid-19, ugonjwa ambao sasa ni janga la kimataifa, sekta mbalimbali ziliathirika.

Kulingana na Muceri, visa vya maambukizi vilivyozidi kuongezeka, mambo yalianza kuenda mrama.

“Baadhi ya wawekezaji katika sekta ya tuktuk walianza kuuza magari yao. Ni gari la jumla ya abiria watano ila Covid iliwashusha hadi wawili,” asema.

Muceri anasema licha ya bidii zake, ukosefu wa mapato ya kutosha kama hapo awali nusra usambaratishe ndoa yake.

“Mke wangu alifikia kiwango cha kushuku nina uhusiano nje ya ndoa, kwa sababu ya mapato kupungua. Pengine alidhani kuna ninayepelekea hela,” aelezea.

“Nakumbuka kuna siku aliniambia ikiwa nimeshindwa kutunza familia nimpashe, ajipange,” aongeza.

Ni matamshi yaliyomkera maini, Muceri akisisitiza alifanya juu chini kunusuru ndoa yake.

Katika mojawapo ya gareji ya tuktuk Githurai, Dickson Muceri akitafuta tuktuk kujiendeleza kimaisha.

Kwa wakati huo walikuwa wamejaaliwa mtoto mmoja pekee, na kwa sasa familia yake imepanuka.

Tangu Kenya iwe mwenyeji wa Covid-19, visa vya vita vya kijinsia na dhuluma katika ndoa vimetajwa kuongezeka.

Hatua hiyo imetajwa kusababishwa na hali ngumu ya maisha.

“Ongezeko hili linatia wasiwasi, tumeandikisha hata zaidi ya mara dufu kipindi hiki cha corona,” anasema Caroline Njuguna, Afisa wa Idara ya Polisi na ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kuangazia visa vya dhuluma za kijinsia.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Utumishi wa Umma, Jinsia na Masuala ya Vijana, visa 5, 009 vya dhuluma za kijinsia viliandikishwa kati ya Januari 2020 – Desemba 2020, kupitia nambari maalum ya 1195.

Ili kutafuta suluhu, kuokoa ndoa yake changa, Dickson Muceri aliamua kupeleka familia yake mashambani, Kaunti ya Meru.

“Niliuza tuktuk na kuanza mradi wa kujenga nyumba ili mke na mwanangu wawe salama,” Muceri afichua, akisema mashambani angalau gharama ya maisha ni nafuu, ila si mteremko vile.

Hata baada ya kurejea jijini Nairobi mapema 2021, kusukuma gurudumu la maisha, mambo hayakuimarika.

Alikodi nyumba ya chumba kimoja eneo la Progressive, Githurai, ila vibarua havipatikani.

Miezi kadha iliyopita, Muceri alijaaliwa mtoto wa pili na lazima ajikaze kiume kukithi familia yake riziki na mahitaji mengine muhimu ya kimsingi.

Maisha ya jiji la Nairobi, hasa baada ya nyongeza ya mafuta ya petroli, kodi ya bidhaa tofauti za kula, mitungi ya gesi, miongoni mwa nyingine, yamekuwa mchongoma kukwea.

Muceri anaiambia Taifa Leo Dijitali ameamua kuhamia eneo la Pwani mwa Kenya, angalau kuona ikiwa mambo yataimarika.

“Ninaendelea kufanya vibarua vinavyopatikana, vikiwemo vya huduma za mikahawa,” asema.

Kwa barobaro huyu ambaye sasa ni baba wa watoto wawili, ni dua kwa Mwenyezi Mungu kasumba ya virusi vya corona itatuondokea kutokana na milima na mabonde aliyopitia.

“Himizo langu kwa wanaopitia hali kama yangu wasilaze damu, wafanye vibarua vilivyopo muradi tu viwe halali,” Muceri ashauri.

Mambo nyanjani si mzaha, katika ukurasa wa mtandao wa WhatsApp wa wawekezaji wa muungano wa wamiliki tuktuk na magari madogo aina ya maruti Githurai (GTMA), ukieleza ubayana wa hali.

Wengi wao wanauza majembe yao ya kazi, kwa sababu ya baishara kuzorota na ugumu wa maisha.

Kisa cha Dickson Muceri, ni kimoja tu kinachoashiria taswira ya mamia, maelfu na mimilioni ya Wakenya waliopoteza nafasi za kazi.

“Ni muhimu serikali ijue Mkenya wa kawaida ndiye anazidi kuumia kupitia ongezeko la kodi, ushuru na kupanda kwa gharama ya maisha,” Peris Mwihaki, mkazi wa Thika na ambaye mwaka huu alipoteza ajira asema.

You can share this post!

Je, mkataba wa kibiashara baina ya Kenya na Uingereza...

Tutaheshimu uamuzi wa mahakama ya rufaa kuhusu BBI –...