Habari Mseto

Corona imesaidia kukabiliana na magonjwa mengine – Serikali

June 15th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Visa vya magonjwa ya kuendesha nchini vimepungua kwa kiwango kikuu, imesema Wizara ya Afya.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe Jumatatu amesema hatua hiyo imechangiwa na kiwango cha juu cha usafi kinachodumishwa ili kudhibiti maenezi ya ugonjwa hatari wa Covid – 19.

“Kwa sababu ya kunawa mikono kila wakati, visa vya magonjwa kama vile ya kuendesha vimepungua. Hata ukiuliza daktari, atathibitisha haya,” Waziri akasema.

Kuzuia maambukizi ya Covid – 19, wizara ya afya ilitoa sheria na mikakati maalum kuzingatiwa. Mikakati hiyo ni pamoja na kuvalia barakoa ndiyo maski katika maeneo ya umma, kunawa mikono kila wakati, kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzake hasa katika umma na pia kuepuka kukongamana.

Hata janga la corona likidhibitiwa nchini, Waziri Kagwe amekariri haja ya wananchi kuendelea kudumisha kiwango cha hadhi ya juu cha usafi. “Udumishaji wa kiwango cha juu cha usafi unapaswa kuwa maisha yetu ya kila siku,” akasema.

Bw Kagwe alisema hayo katika ziara yake eneo la Nyandarua, ambako alikuwa amezuru kaunti hiyo kutathmini maandalizi yake katika kukabiliana na Covid – 19.

Kipindupindu na Homa ya Matumbo ni baadhi ya magonjwa yanayosababishwa na uchafu.