Michezo

Corona imetufilisiha, yasema Barca

August 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

RAIS wa Barcelona, Josep Maria Bartomeu amesema “itakuwa vigumu sana” kwa miamba hao wa soka ya Uhispania (La Liga) kumsajili upya mvamizi Neymar Jr kutoka Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kutokana na hali mbaya ya kifedha ambayo imechangiwa na corona.

Aidha, amefichua kwamba mipango ya kumsajili fowadi Lautaro Martinez, 22, kutoka Inter Milan pia imesitishwa. Martinez alitazamiwa kutua uwanjani Camp Nou mwishoni mwa msimu huu ili kujaza pengo la kigogo Luis Suarez ambaye mkataba wake unatamatika mwishoni mwa 2021.

Kwa mujibu wa gazeti la Sport nchini Uhispania, habari hizo zinatarajiwa kuwavunja moyo wanasoka wengi ambao wamekuwa na matamanio ya kuingia katika sajili rasmi ya Barcelona mwishoni mwa msimu huu.

Kwa kipindi cha miezi minne pekee kati ya Machi na Juni 2020, Bartomeu amekiri kwamba Barcelona wamepoteza jumla ya Sh25 bilioni kutokana na janga la corona.

“Vikosi vyote vya haiba kubwa katika soka ya bara Ulaya vimeathiriwa. Hili janga ambalo sidhani litakuwepo tu kwa mwaka mmoja na kutoweka. Litakuwa nasi kwa muda, pengine miaka mitatu au hata minne na ni pigo kubwa,” akaongeza kinara huyo.

Neymar ambaye ni fowadi mzawa wa Brazil alijiunga na PSG kwa kima cha Sh26 bilioni mnamo Agosti 2017 baada ya kuagana na Barcelona waliojaribu kumsajili upya mwishoni mwa msimu uliopita wa 2018-19.

“Neymar? Katika hali hii ya sasa, haiwezekani kabisa kumsajili,” akasema Bartomeu.

“Na sidhani kwamba PSG watataka kumtia mnadani kwa sasa kutokana na ukubwa wa mchango wake kikosini. Barcelona wamezungumza na Inter Milan na wameafikiana kusitisha kabisa mazungumzo kuhusu usajili wa Martinez kwa kuwa hali yetu ilivyo kwa sasa haiwezi kuturuhusu kujinasia huduma za wanasoka ghali wa kiwango chake,” akaendelea Bartomeu.

“Katika msimu wa 2020-21, tulitarajia kuvuna angalau Sh123 bilioni kutokana na shughuli za kibiashara na ushindi wa mataji muhimu. Sasa huenda tukajizolea takriban asilimia 30 pekee ya fedha hizo kwa kuwa biashara nyingi zitakwama.”

“Iwapo hali ya corona haitabadilika, basi ina maana kwamba tutazidi kukosa mashabiki, makavazi yatasalia kufungwa, maduka yetu hayatakuwa wazi na fedha nyingi zitapotea. Huu ni ukweli ambao unatufanya kuwazia upya namna na mahali pa kuwekeza haraka na kuteua miradi inayoweza kusubiri hadi hali itakavyorejea kuwa kawaida bila ya kikosi pia kuathirika zaidi.”

Bartomeu pia alithibitisha kwamba Barcelona wameanzisha mchakato wa kisheria dhidi ya kiungo Arthur Melo ambaye kwa sasa anatazamiwa kujiunga rasmi na Juventus huku nafasi yake ugani Camp Nou ikitwaliwa na kiungo mzawa wa Bosnia, Miralem Pjanic.

“Tulikuwa na maagano na Melo kwamba atasalia kuwa mchezaji wetu hadi baada ya kutamatika kwa kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu. Angetusaidia sana kunyanyua ufalme wa kipute hicho. Lakini hakurejea tangu shughuli za soka zilizokuwa zimesitishwa na corona kuanza upya,” akasema Bartomeu ambaye amekuwa rais wa Barcelona tangu 2014.

Bartomeu amefichua pia mpango wa kuwatia mnadani wanasoka tisa mwishoni mwa msimu huu wakiwemo Rafinha, Ivan Rakitic, Arturo Vidal, Nelson Semedo, Junior Firpo, Todibo na Samuel Umtiti anayehusishwa pakubwa na Arsenal na Manchester United.