Corona: Kagwe atoa afueni kwa kaunti 13 za magharibi mwa Kenya

Corona: Kagwe atoa afueni kwa kaunti 13 za magharibi mwa Kenya

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI sasa imebadilisha saa za kafyu katika kaunti 13 katika maeneo yanayopakana na Ziwa Victoria ambayo yalitajwa kuwa yenye visa vingi ya maambukizi ya corona.

Akiongea na wanahabari jijini Nairobi, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe alisema Ijumaa kuwa amri hiyo ya kutotoka nje sasa itaanza kutekelezwa kuanzia saa nne za usiku hadi saa kumi alfajiri, sawa na maeneo mengine ya nchi.

Kwa kipindi cha siku 29 zilizopita, saa za kafyu katika kaunti hizo za magharibi mwa Kenya zimekuwa zikianza saa moja jioni hadi saa kumi alfajiri. Hii ni kufuatia kupanda kwa visa vya maambukizi ya virusi vya corona kuanzia mwezi jana

Kaunti zilizowekewa sharti hili ni; Kisumu, Kakamega, Siaya, Bungoma, Busia, Kisii, Nyamira, Migori, Homa Bay, Bomet, Kericho, Vihiga na Trans Nzoia.

“Saa za kafyu inayoendelea kuzingatiwa nchini zitasalia zilivyokuwa awali, kuanzia saa nne za usiku hadi saa kumi alfajiri. Saa hizi pia zitazingatiwa katika kaunti 13 za eneo la ziwa ambazo awali zilikuwa zimetajwa kwa pamoja kama eneo lenye maambikizi ya juu ya virusi vya corona,” Bw Kagwe akawaambia wanahabari nje ya jumba la Harambee jijini Nairobi.

Waziri ambaye alikuwa ameandamana na Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua, kwa mara nyingine aliwaonya Wakenya dhidi ya kulegeza masharti ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa.

“Katika siku za hivi karibuni idadi ya visa vipya vinavyokakiliwa kila siku imeongezeka sawa na wagonjwa wanaohitaji kulazwa katika ICU na wale wanaotaka kupewa oksijeni ya ziada. Hali hii inachangia na hatua ya baadhi ya Wakenya kuanza kulegeza kanuni zilizoweka na wanasiasa kurejelea mikutano ya hadhara,” akasema Bw Kagwe.

“Nawaomba Wakenya kuchukua jukumu la kibinafsi kwa kuendelea kuzingatia kanuni zilizowekwa. Komeni kuhudhuria mikutano ya wanasiasa. Ikiwa unavutiwa kwenda huko na pesa, nenda ukachukue pesa kisha rejea nyumbani usije ukaambukizwa corona,” akaongeza.

Waziri pia aliwataka waajiri kuwaruhusu wale wahudumu kufanyia kazi nyumbani “ikizewekana ili kupunguza msongamano sehemu za kazi.

Bw Kagwe pia aliamuru kwamba maiti zizikwa baada ya saa 72 ili kuzuia uwezekano na watu kukongamana kwa muda mrefu wakipanga mazishi.

You can share this post!

Wanasiasa wakuu watatii kanuni au wataendelea kupepeta...

Agala na Makokha wamaliza voliboli ya ufukweni Olimpiki...