Habari Mseto

CORONA: Kaunti zaendelea kuweka mikakati

March 16th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

KAUNTI Jumatatu ziliendelea kuweka mikakati ya kudhibiti maenezi ya virusi vya corona siku moja baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutoa maagizo makali kwa lkengo la kulinda Wakenya.angaza tahadhari kadha zitakazozingatiwa nchini.

Baadhi ya hatua ambazo kaunti zimechukua ni kupiga marufuku soko za wazi, kufunga shule za chekechea na vyuo vya kiufundi, pamoja na kuzuia watu kutembelea wagonjwa hospitalini.

Baadhi ya mabunge ya kaunti yalisitisha vikao kwa muda, katika juhudi za kupunguza hali ya watu wengi kukongamana, ambayo inahatarisha uenezaji wa ugonjwa huo.

Katika Kaunti ya Kakamega, Gavana Wycliffe Oparanya pia alipiga marufuku wakazi kupeleka maiti katika hifadhi za maiti, badala yake akiwataka kuwazika muda mfupi baada ya kuaga.

Bw Oparanya aliwataka walio na wafu mochari kwenda kuwachukua, akisema serikali ya kaunti hiyo ilikuwa imeondoa gharama zote za maiti zilizokuwa mochari.

“Hatutapokea miili tena katika mochari za umma, lakini tutasaidia familia zilizo na wafu kuwazika haraka iwezekanavyo,” akasema.

Gavana huyo alisema kamati ya watu sita ikiongozwa naye iliundwa kusimamia masuala yote kuhusu corona, Sh110 milioni zikatengwa kwa matayarisho endapo utazuka na madaktari 232 kupewa mafunzo.

Vilevile, gavana huyo alipiga marufuku soko za wazi, makundi ya wahudumu wa bodaboda na kufunga shule za chekechea na vyuo vya kiufundi, sawa na Gavana wa Narok, Bw Samuel Tunai ambaye pia alifunga soko zote za wazi na kuwataka wahudumu wa bodaboda na matatu kunawisha wateja wao.

Bw Tunai pia aliamrisha baa na vilabu vyote vya usiku kufungwa kwa siku 30, akisema ni katika biashara hizo ambapo watu wengi hupatana na ambapo ugonjwa unaweza kusambaa.

Gavana huyo pia alisema kaunti imetuma maafisa wa afya sehemu za kuingia na kutoka katika mbuga ya kitaifa ya Maasai Mara kupima ikiwa watalii wana virusi vya corona, akisema vitanda 20 katika hospitali mbili za umma vimetengwa iwapo kuna watu wataripotiwa kuugua ugonjwa huo.

Katika Kaunti ya Nairobi, bunge la kaunti lilisitisha vikao kwa siku 30, huku idara ya afya katika serikali ya kaunti ikisema ilikuwa imeanzisha utoaji mafunzo kuhusu corona kwa watu, katika vituo vya mabasi, vya afya na afisi za umma.

Katika Kaunti ya Makueni vilevile, soko za wazi zilipigwa marufuku, vyuo vya kiufundi kufungwa na wahudumu wa bodaboda na matatu wakihitajika kuwanawisha wateja mikono.

Naye Gavana wa Nandi, Bw Stephen Sang aliagiza wafanyakazi 4,000 kufanyia kazi nyumbani kwa mwezi moja kama mbinu ya kupunguza msongamano, ingawaje wale wa idara za afya na fedha wataendelea kufika afisini.

Katika Kaunti ya Vihiga, vituo vya kupima watu waliokuwa wakiingia huko ugonjwa huo viliwekwa, ili kuhakikisha kila aliyeingia hakuwa mwathiriwa.

Nako jijini Mombasa, wakazi walikuwa wakihofia kuwa virusi vya corona huenda vikaenea sana katika kivuko cha feri Likoni, ambacho hutumika na maelfu ya watu wakisafiri kati ya Mombasa na Kusini mwa Pwani.

Wakazi hao walilaumu Shirika la kutoa Huduma za Feri (KFS) kuwa halikuweka mikakati ifaayo ili kuwakinga abiria kutokana na maambukizi ya ugonjwa huo.