Corona: Kifo cha polisi chaanika mahangaiko

Corona: Kifo cha polisi chaanika mahangaiko

Na MAUREEN ONGALA

MASAIBU ambayo wagonjwa wa Covid-19 hupitia katika kaunti za Pwani, yameanikwa wazi baada ya kifo cha afisa mkuu wa usalama wa Chuo Kikuu cha Pwani, Bw Samuel Kiponda.

Imebainika kuwa, Bw Kiponda alifariki katika uwanja mdogo wa ndege wa Vipingo, alipokuwa akisubiri kusafirishwa hadi Nairobi baada ya kukosa chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali zote za Pwani.

Alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti Kilifi kwa siku mbili akipokea matibabu, akafariki Agosti 17 na kuzikwa wikendi iliyopita.

Kulingana na Bi Quinter Rimba ambaye ni mmoja wa wahudumu wa afya waliyemwuguza afisa huyo alipokuwa hospitalini, maisha yake yangeokolewa kama kungekuwa na kifaa cha kumsaidia kupumua.

“Wakati mwingine huwa inabidi tu daktari afe moyo kwa juhudi zake nyingi za kuokoa maisha ya mgonjwa, na amwachie Mungu. Bw Kiponda alipigania maisha yake. Kiwango chake cha oksijeni kilikuwa sawa, lakini hakikutosha. Alikuwa amedhoofika na alihitaji mashine ya kumwongeza hewa mwilini,” akasema.

Bi Rimba alieleza kuwa, walijitahidi sana kutafuta chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali zote walizotarajia kupata Pwani lakini hawakufua dafu.

“Kaunti ya Kilifi haina ICU. Kama ingekuwepo, tungeokoa maisha. Tulihitaji tu mashine ya kumwongeza hewa wakati huo. Tatu zilizokuwepo zilikuwa zinatumiwa na wagonjwa wengine, na ya nne haiwezi kutumika kwa sababu muundo wake hauambatani na vifaa vingine vinavyohitajika kuunganishwa nayo,” akasema.

Idara ya Kitaifa ya Huduma za Polisi ilifanikiwa kupata chumba cha ICU katika Hospitali ya Nairobi West iliyo Kaunti ya Nairobi, na madaktari wa Hospitali ya Kilifi wakakamilisha maandalizi yote ya kumhamisha.

Ndege iliyotarajiwa kumsafirisha kutoka Kilifi hadi Nairobi ilifaa kutua katika uwanja mdogo wa ndege wa Vipingo saa tisa unusu mchana, lakini akafariki dakika 45 kabla wakati huo ufike.

Alisihi jamii kufuata kanuni za kuepuka maambukizi ya virusi vya corona, akionya kuwa wengi watakuwa hatarini kufariki kwa sababu ya ukosefu wa vyumba vya kutosha vya wagonjwa mahututi.

Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, alifungua kitengo maalumu cha matibabu ya Covid-19 mnamo Julai mwaka uliopita.

Wakati huo, serikali ya kaunti ilisema ilinunua vitanda saba vya ICU na mashine saba za kusaidia wagonjwa waliolemewa kupumua.

Hata hivyo, kitengo cha ICU bado hakijaanza kutumiwa.Katibu wa Kaunti ya Kilifi, Bw Arnold Mkare, alikiri kuwa utawala wa kaunti hiyo haujawahudumia vyema wananchi kiafya.

“Jukumu langu kuu ni kutetea msimamo wa serikali, lakini kwa hili, imenibidi nikubali udhaifu wetu serikalini,” akasema.

Alilaumu hali inayoshuhudiwa kwa ufisadi miongoni mwa baadhi ya maafisa wa kaunti wanaodaiwa walinunua vifaa vibovu vya matibabu, akasema serikali ya kaunti itajitahidi kutatua changamoto zilizopo.

“Idara ya afya ilinunua vifaa vya kupambana na ugonjwa wa Covid-19 kwa mamilioni ya pesa, lakini mashine hizo zina hitilafu. Tulipoteza pesa hivyo tu,” akasema.

Madai hayo ya ufisadi katika idara ya afya ya kaunti yanaendelea kuchunguzwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

You can share this post!

Spark FC yacharaza Real Stars katika mojawapo ya matokeo...

WANDERI KAMAU: Wanawake ni thawabu kuu tunayofaa kujivunia