Michezo

CORONA: Kiungo wa Harambee Starlets amaliza karantini

March 24th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KIUNGO matata wa timu ya taifa ya soka ya Kenya, Jentrix Shikangwa ameelezea furaha yake baada ya kukamilisha muda wa kujitenga wa siku 14.

Shikangwa alilazimika kuwa chini ya karantini baada ya kuzuru Uturuki wiki chache zilizopita.

Katika mahojiano na Taifa Spoti, kiungo huyo alisema hali yake ni shwari na kwamba yuko tayari kurejelea mazoezi.

Shikangwa alisaidia Harambee Starlets kutwaa taji la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya mwaka jana. Alifunga mabao 10 katika kipute hicho kilichoandaliwa nchini Tanzania.

Mchezaji huyo alikuwa katika kikosi kilichoelekea nchini Uturuki kati ya Machi 2-11 kwa kipute cha Turkish Women’s Cup.

Starlets inayonolewa na kocha David Ouma ilimaliza mashindano hayo ya timu nane katika nafasi ya tatu, na kutwaa nishani ya shaba. Chile na Ghana zilizoa medali za dhahabu na fedha, mtawalia.

Baada tu ya kurejea nyumbani, serikali ilitangaza kuwa watu wote walioingia nchini Kenya katika siku 14 zilizopita wajitenge ili kuzuia uenezaji wa virusi hatari vya corona.

“Hatujakuwa tukifanya mazoezi kwa muda sasa. Nafurahi kumaliza karantini. Niko tayari kuanza mazoezi,” alisema chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 18 kwa njia ya simu kutoka Sigalagala katika Kaunti ya Kakamega.

Shikangwa, ambaye ni mwanafunzi katika Shule ya Upili ya Wiyeta, alisema kuwa atafanya mazoezi na timu ya wavulana ya Shipala.

Aidha, amezungumzia ziara ya Uturuki akieleza kuwa, mbinu za Kenya za kuzuia badala ya kushambulia timu pinzani hazikuwaisaidia pakubwa katika mashindano hayo.

“Nilifurahia safari ya Uturuki lakini sikuridhika timu yetu kukamilisha mashindano nambari tatu. Ni kweli tulikutana na timu ambazo zina uzoefu na wachezaji walio na ujuzi mkubwa kimataifa.

“Lakini pia sisi hatukuwa wazuri katika umilikaji wa mpira na kusaka magoli. Sioni kama mbinu zetu za kuzuia badala ya kufanya mashambulizi, zilifanya kazi. Tunapenda sana kuzuia na mbinu hii ilifanya ngome yetu kushambuliwa sana, tukaishia kufungwa mabao na Chile (5-0) na Ghana (3-1),” alikariri mwanadada huyo ambaye pia anachezea klabu ya Vihiga Queens kwenye Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL).

Starlets ilichabanga Northern Ireland 2-0 katika mechi ya kundi lake, matokeo ambayo yaliiwezesha kukamilisha makala hayo ya tatu katika nafasi ya tatu.

Vipusa hao wa Kenya walikuwa wamealikwa kushiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza kabisa, na waliyatumia kujiandaa kwa mechi za kufuzu kwa Kombe la Afrika (AWCON).