Habari Mseto

CORONA: Kizaazaa Nakuru madereva na wanabodaboda wakifurushwa

March 27th, 2020 2 min read

Na SAMUEL BAYA

KULIZUKA kizaazaa mjini Nakuru polisi walipolazimika kuwafurusha madereva wa matatu na wanabodaboda ambao walikuwa wamekaidi agizo la maafisa wa usalama kutoingia mjini humo katika juhudi za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Polisi hao walipuliza vingora katika magari yao huku wakiwafukuza madereva wajeuri ambao walikaidi agizo hilo.

Jumatano, kamati maalum iliyoundwa kukabili janga la virus vya corona katika kaunti ya Nakuru lilitangaza mikakati kadhaa kukabili hali hiyo.

Kamati hiyo inaongozwa na Gavana wa Nakuru Bw Lee Njiru na kamishna wa kaunti Bw Erastus Mbui.

Baadhi ya mikakati ambayo iliwekwa na kamati hiyo ni kutoruhusu matatu na pikipiki kufika mjini, pamoja na kuhamisha shughuli za soko kutoka katikati ya mji hadi katika uwanja wa michezo wa Afraha.

Maafisa wa usalama washika doria katika barabara kuu za kuingia mjini ili kuhakikisha wachuuzi na waendeshaji bodaboda hawaingii mjini. Picha/ Richard Maosi

Polisi walizunguka kwa malori katikati ya mji wa Nakuru huku wakiwataka wale ambao hawana shughuli yoyote kubakia nyumbani katika hali ya kusimamisha kuenea kwa virusi hivyo hatari.

Baada ya hekaheka hizo kutulia, maafisa wa usalama pamoja na wahudumu wa afya wa kaunti walianza mpango wa kunyunyizia dawa maduka na maeneo yote mjini katika harakati za kukabiliana na kuenea kwa virusi hivyo.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari baada ya kuzindua mpango huo wa kunyunyizia dawa, afisa mkuu wa masuala ya afya katika kaunti hiyo Dkt Samuel King’ori alisema kaunti imeweka mikakati mingi ikiwemo kuweka maji safi katika kila eneo ili wananchi waweze kunawa mikono na kuzuia maambukizi ya virusi hivyo.

“Tutazunguka na kumwaga dawa kote mjini Nakuru, katika meeno ya soko, vituo vya magari na mitaani na hata katika sebule za benki.

Shughuli za usafiri zimesimama wakati huu ambapo steji zimebakia mahame bila wasafiri, wengi wao wakiamua kubakia majumbani pao. Picha/Richard Maosi

“Vile vile tuandeleza mpango wa kuingia nyumba hadi nyumba kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa kujikinga dhidi ya vurisi hivi hatari,” akasema Dkt Kingori.

Aidha alitangaza kurudi kazini mara moja kwa maafisa wote ambao walikuwa katika likizo huku akisema kuwa serikali ya kaunti itachukua kila hatua kuhakikisha kwamba hakuna visa vya maambkuzi kutokea.

“Hivi tunavyongea, serikali ya kaunti inaendeleza mpango wa kuwafunza madaktari kutoka chuo kikuu cha Moi, Eldoret kuhusu jinsi ya kufuatilia kuhusu virusi hivi na hatua ambazo weanafaa kuchukua,” akasema.

Dkt Kingori alisema kuwa vifaa vya kuosha mikono na bidhaa nyengine za usafi vimepelekwa katika hospitali zote katika kaunti huku serikali hiyo pia ikigawa maji ya bure ili kuwezesha wananchi wasafishe mikono.

“Lazima tuwe makini na kuhakikisha kwamba virusi hivi haviingii huku kwetu. Na siri ya haya yote ni moja tu. Lazima tuzingatie usafi maana hilo ndilo jambo muhimu kwa sasa,” akasema.

Wahudumu kutoka kaunti ya Nakuru waanza rasmi kupulizia kila mahali dawa ili kukabili maambukizi ya coronavirus. Picha/ Richard Maosi

Kamati hiyo maalum ilipendekeza kuwa boda bod azote hazitaruhusiwa kuingia mjini na pia haziruhusiwi kamwe kubeba mtu yeyote. Vile viel wauzaji reja reja pia walipigwa marufuku katikati ya mji huku matatu pia zikitolewa mjini na kuammuriwa zibebe abiria kutoka nje ya mji.

Bw Mbui katika taarifa yake alisema kuwa mikakati hiyo ilichukuliwa na kaamti yake baada ya kugundua kwamba wakenya walikuwa hawataki kusikiliza yale ambayo serikali inasema.

“Kufeli kwa umma kusikiliza ile mipango ambayo serikali imeweka katika juhudi za kukabiliana na Corona ndio jambo ambalo lilifanya tuanze mikaakti hii. Hatuwezi kuhatarisha maisha yetu wenyewe na lazima tujichunge,” akasema Bw Mbui.