Michezo

Corona kuvuruga kalenda ya soka ya kimataifa kwa hadi miaka mitatu

May 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

COVID-19 huenda ikaathiri kalenda ya soka ya kimataifa kwa kipindi cha miaka miwili au mitatu.

Haya ni kwa mujibu wa Lars-Christer Olsson ambaye ni mwanachama wa kamati ya soka ya bara Ulaya (Uefa).

Olsson ambaye pia ni Rais wa Ligi za Ulaya, amesema kwa sasa itakuwa ni suala la kusubiri na kuona hali itakavyokuwa ili kuweza kutathmini athari za janga la corona katika mapambano mbalimbali, zikiwemo fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

Uefa ina matumaini ya kumaliza kampeni za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Europa League mnamo Agosti 2022.

Uamuzi wa iwapo hilo linawezekana au la unatarajiwa kutolewa Mei 18, 2020.

Pia kuna mipango ya kuratibu michuano mara tatu badala ya mara mbili katika ngazi ya soka ya kimataifa kama vile Euro 2020, michuano ya ligi ya taifa na mechi za kirafiki.

Kwa mujibu wa Olsson, itakuwa heri zaidi msimu wa sasa usimalizike badala ya kuchelewa kuanza kampeni za msimu ujao.

“Sina shaka kwamba kalenda yetu itaathirika kwa miaka miwili au mitatu,” akasema Olsson akitoa maoni yake kuhusu kusitishwa kwa michezo ya soka katika nchi mbalimbali na pia kuahirishwa michuano ya Euro 2020.

Awali, alikuwa ameshikiliwa kwamba hakuna maridhiano miongoni mwa mataifa kuhusu michuano ya ndani ya nchi, kwa sababu kila nchi inakabiliwa na hali tofauti baada ya kuathiriwa na janga la corona kwa viwango tofauti.

Ligi mbili za hadhi ya juu nchini Ufaransa, Ligue 1 na Ligue 2, hazitarejelelewa kabisa msimu huu baada ya Ufaransa kupiga marufuku michezo yote licha ya mapendekezo kwamba ichezewe ndani ya viwanja vitupu hadi Septemba 2020.

Ligi ya Uholanzi ilisitishwa wiki jana huku kukikosekana klabu iliyopandishwa daraja, kushushwa ngazi wala kutangazwa mshindi.

Alipoulizwa kuhusu utaraibu wa kushirikisha PSG na Ajax, katika kipute cha UEFA baada ya ligi za Ufaransa na Uholanzi kuhitimishwa, Olsson alisema, “Hili ni jambo gumu kulizungumzia lakini katika hali yoyote ile, masuala yasiyo ya kawaida huhitaji utatuzi usio wa kawaida.”

“Kwa sasa tunaendelea na mipango, tunajaribu kupiga hatua katika kufanikisha maandalizi ya mechi zilizosalia msimu huu katika kipindi cha mwezi mmoja wa Agosti,” akatanguliza.

“Kama hilo litafanikiwa, basi nafikiri tutaweza kuhifadhi uhalisia wa michuano yote ya kimataifa ya kandanda. Itatupasa kurejelea kampeni hizi kufikia mwishoni mwa Mei kwa sababu zaidi ya hapo, hakika itakuwa vigumu kwa mipango hii kufaulu,” akaongeza.

Huku ikisalia miaka miwili pekee kwa michuano ya Kombe la Dunia kufanyika, Olsson anakiri kwamba kutakuwa na matatizo makubwa katika kalenda ya kimataifa.

“Pale ambapo baadhi ya michuano itaahirishwa kwa mwaka mmoja zaidi katikati ya msimu, hapo kutakuwa na athari. Lakini nafikiri kwanza inatupasa kusubiri na kuona ni kwa namna gani athari hizi zitaendelea,” akasisitiza.