Habari Mseto

CORONA: Magereza ya Thika yanyunyiziwa dawa

April 3rd, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KAUNTI ya Kiambu chini ya idara ya Afya ya umma iliendesha zoezi la kunyunyiza dawa katika gereza la Thika Ijumaa.

Maafisa wa afya ya umma walichukua jukumu la kuwahamasisha maaskari wa jela, na wafungwa ili wajizuie na Homa ya Covid -19.

Afisa mkuu wa jela hiyo Bw Billy Koshal, alipongeza juhudi hiyo akisema litawapa mwelekeo mwema wa kujikinga na homa hiyo ya Corona.

“Tunapongeza juhudi iliyotekelezwa na kaunti ya Kiambu kwani ni njia moja ya kujali maslahi ya wafungwa jela ya Thika,” alisema Bw Koshal.

Alisema maafisa wake wanaendelea kuwahamasisha wafungwa umuhimu wa kunawa mikono kila Mara na kuhakikisha wanadumisha usafi kila Mara.

“Kwa wakati huu changa moto kuu kwa wafungwa hawa ni ukosefu Wa sabuni na karatasi za kwenda msalani.Hata hivyo tunajaribu kukabiliana na shida hiyo,” alisema Bw Koshal.

Tayari serikali imepiga marufuku kutembea magerezani ili kuzuia maabukizi ya homa ya Corona.

Kaunti ya Kiambu imeanza zoezi la kunyunyizia dawa kila sehemu ili kukabiliana na homa hiyo.

Baadhi ya maeneo yaliyonyunyiziwa dawa ni kwenye masoko, vituo vya polisi na vituo vya magari.

Tayari gavana wa Kiambu Dkt James Nyoro alitoa amri idara ya Afya ya umma ifanye hima kunyunyizia dawa katika Miji mikuu katika kaunti hiyo.

Alisema tayari amezuru hospitali kuu za Kiambu na kuridhika jinsi wanavyoendesha shughuli zao.

Gavana hiyo alizuru hospitality ya Thika Level 5, Kiambu Level 5, na Gatundu Level 5.

Hospitali hizo zimetenga wadi maalum za kuwaweka wagonjwa watakaopatikana na homa ya Corona.

” Kwa muda wa wiki moja nimezunguka maeneo mengi na nimerithika jinsi wananchi wanavyo dumisha usafi,” alisema Dkt Nyoro.

Tayari kampuni kadhaa na washika dau wamejitokeza na kutoa Mutungi za maji na dawa za vieuzi ( sanitizer) ili kusaidia wananchi popote walipo kuzuia Homa ya Covid-19.

Baadhi ya kampuni hizo ni Thiwasco Water Company, Bidca Africa Ltd, Equity Bank, Mama Millers, Visha Oshwal Community, na wahisani wengine wengi.