Habari Mseto

CORONA: Maisha mitaa ya mabanda ni kawaida

March 18th, 2020 1 min read

SAMMY KIMATU Na EUNICE MURATHE

HUKU hatari ya virusi vya corona ikitishia kulemaza maisha ya kawaida, baadhi ya watu wanaendelea kupuuza janga hilo.

Katika eneo la Viwandani jijini Nairobi, matatu za kuhudumu kutoka Muthurwa hadi Lunga Lunga jana hazikuwa na sabuni ya kutumiwa na abiria.

Katika mitaa ya Mukuru, shughuli za kila siku ziliendelea kama kawaida huku watu wakisalimiana kwa mikono kama kawaida.

Vilabuni, vioski na bucha pia hakukuwa na sabuni.Katika Kaunti ya Mombasa, wakazi hawajaanza kutilia maanani unawaji mikono hasa katika mitaa ya mabanda.

Ndani ya mtaa wa Bangladesh ulio na watu zaidi ya 2,000, uhaba wa maji umekithiri, na mitaro ya maji chafu imezagaa.

“Hatuna maji ya kutosha hapa. Tunayopata ni ya kunyua na ya matumizi nyumbani. Corona ikifika hapa, tutakuwa taabani,’ Bi Emma Onyango akasema.Katika mtaa wa mabanda wa Muoroto, wakazi walilaalamikia bei ya juu ya maji.

“Mimi naishi maisha ya kawaida. Serikali iliruhusu ugonjwa wa corona kuingia Kenya. Ni vigumu mno kwangu kuacha kusalimiana kwa mikono. Maji mjini Mombasa ni ghali,’ Bw Kilonzo akasema.

Sokoni Muthurwa jijini Nairobi, muuzaji wa samaki Rose Luis alisema wengi wa wateja pamoja na wauzaji hawanawi mikono.“Serikali itusaidie kwa sababu kugharamia sabuni ya kunawa kila wakati ni gharama ya ziada kwa walio wa mapato ya chini,” akasema.

Wizara ya Afya nayo imeanza kuweka mifereji ya maji katika maeneo mbalimbali yanayotumiwa na umma. Mafundi jana walikuwa wakiweka mifereji katika kituo cha mabas cha Bus Station.

Maduka makubwa ya Supermarket nayo yaliweka mikakati ya kuzuia virusi vya corona.Ndani ya Eastmatt Supermarket jijini Nairobi, keshia walivalia vitambaa midomoni na glavu mikononi wakihudumia wateja.

Meneja katika tawi hilo Joke Oyunge alisema wananawisha kila mteja kabla ya kuruhusiwa kuingia dukani.Katika duka la Naivas Moi Avenue, meneja Martin Muturi alisema wameweka sabuni ya kunawa kila eneo.