Makala

CORONA: Mapasta na wafuasi wao waumia

March 24th, 2020 3 min read

Na GEOFFREY ANENE

VIRUSI vya corona vimeumiza binadamu na sekta nyingi za maisha yake bila ya kubagua ukiwemo uchumi wa makanisa.

Mwandishi huyu alipata kuzungumza na waumini kadhaa kuhusu jinsi virusi hivyo vimeathiri makanisa yao na shughuli za makanisa.

Rodgers kutoka kanisa la Charismatic Episcopal Church of Kenya (CEC Kenya) anasema wachungaji ndio wataumia zaidi.

“Katika kanisa letu, watumishi wote wanategemea sadaka ya waumini kulipwa mshahara. Tunaheshimu agizo la serikali la kutaka tusiende makanisani kwa sababu ya kuzuia maambukizi ya corona.

“Hata hivyo, wachungaji sasa wasahau mishahara hadi pale hali ya kawaida itarejelewa. Kwa sababu idadi ya waumini katika parokia yetu ni ndogo, matoleo ya kila Jumapili huwa angaa Sh2,500 kutegemea na jinsi wamehudhuria ibada.

“Kutoka kwa sadaka hii, pia kutegemea jinsi ilivyotolewa katika Jumapili hizo nne, tunalipa padre kati ya Sh2,000 na Sh7000 kama mshahara kwa mwezi,” anasema Rodgers kutoka kaunti ya Kakamega.

Juddy kutoka kanisa la Divine Mercy jijini Nairobi anasema, “Marufuku dhidi ya kuenda kanisani inatuathiri sisi sote, ingawa watumishi ndio wataumia zaidi kifedha. Sisi hutoa sadaka ya zaidi ya Sh20,000 kila Jumapili. Sina uhakika kama waumini watatuma sadaka hii kupitia huduma za M-Pesa. Sidhani kama njia hiyo ya kutuma sadaka itafaulu kwa sababu pia wengi hawajakumbatia teknolojia ya kidijitali.”

Naye Ngome kutoka Trans-Nzoia anasema ameshangazwa na hatua ya waumini wa kanisa la African Church of Holy Spirit (Avaushi) kupuuza agizo la serikali la kutaka wajiepushe na mikusanyiko mikubwa kama inayoshuhudiwa makanisani.

“Kwao, virusi vya corona ni kitu ambacho hakiwezi kuwafikia wala kuwaathiri. Jumapili iliyopita, niliona waumini wakimiminika humo baada ya kuimba na kupiga ngoma kwenye foleni kando ya barabara. Walisalimiana kwa mikono na kupiga pambaja kama kwamba virusi vya corona havijafika Kenya.

“Serikali inahitajika kuingilia kati, la sivyo naona sis hapa tumekalia bomu inayoweza kulipa wakati wowote,” anasema kabla ya kufichua kuwa kila Jumapili, sadaka kwenye kanisa hili huwa kati ya Sh20, 000 na Sh30, 000.

Abigail, ambaye anashiriki katika kanisa la Kikatoliki mtaani Ngong, na Charles kutoka Winners Chapel mjini Nairobi, wanasema makanisa yao yameathirika vibaya, ingawa hawajui yaliyoumizwa kiuchumi.

Hata hivyo, Charles anaongeza, “Kutoa sadaka ni kitu cha kawaida, ingawa sisi tunafanya hivyo kupitia huduma za M-Pesa kwa sababu ibada zetu zinaendeshwa kupitia mitandao kutoka makao makuu nchini Nigeria.”

Wasike kutoka kanisa la Deliverance Church anasema kuwa anaunga mkono watu kujitenga ili kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kwa sababu “fedha si muhimu kuliko maisha.”

“Wakati huu, kila sekta inaumia kiuchumi. Watu wanapoteza kazi na kwa hivyo makanisa hayafai kuwa yanawazia jinsi ya kuimarika kifedha wakati huu. Sijui kiasi cha sadaka ambacho sisi hutoa, lakini najua ni kikubwa. Hata hivyo, kuabudu fedha tunafahamu ndicho chanzo cha maovu yote.”

Askofu wa WorshipLand Miracle Church Dandora, Alphonce Wandera anasema uchumi umeharibika katika sekta zote ikiwemo kanisa na kuomba Mungu aondolee Kenya janga la virusi vya corona. “Sadaka hakuna. Sadaka inasaidia katika njia nyingi ikiwemo watu wasiojiweza na miradi ya kanisa. Hatuna mapato mengine isipokuwa sadaka kwa hivyo shughuli zetu zimekwama,” anasema.

Mwaka 2019, tovuti moja nchini Kenya iliripoti kuwa makanisa ya Christ is the Answer Ministries, Nairobi Chapel, Mavuno Church, All Saints Cathedral na Nairobi Baptist yanashikilia nafasi tano za kwanza katika orodha ya makanisa tajiri yanayopata mamilioni ya shilingi kila mwaka kama mapato.

Kufuatia amri ya Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya mikusanyiko iliyoshuhudia pia maeneo mengine ya kuabudu yakiathiriwa na marufuku hiyo, makanisa ‘mabwanyenye’ na mengi yanayopata matokeo ya chini yanatarajiwa kuumia kiuchumi wakati huu.

Waumini wanasalia nyumbani ili kujizuia kupata virusi hatari vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19, ambao umeambukiza watu 384, 000 tangu uanzie mjini Wuhan nchini Uchina zaidi ya miezi miwili iliyopita. Virusi hivyo vimesababisha vifo vya watu 16, 591.

Visa 16 vimethibitishwa nchini Kenya, ingawa hakuna mtu aliyepoteza maisha kutokana na virusi hivyo.