Habari Mseto

CORONA: Mkenya anayeishi Italia asimulia maisha yalivyobadilika

April 6th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

ITALIA ni mojawapo ya mataifa yaliyoathirika sana na maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona.

Kufikia Aprili 6 asubuhi, ilikuwa imeshuhudia visa 128, 948 vya maambukizi ya ugonjwa huo hatari ambao umeua watu 69,758 kote duniani. Watu 15, 887 wameaga dunia nchini Italia pekee.

Mwandishi huyu alipata kuzungumza na Mkenya James Barasa anayeishi mjini Verona kufahamu hali ilivyo katika mji huo na jinsi maisha yake yamebadilika tangu visa vya virusi vya corona vithibitishwe nchini humo.

Hii hapa hadithi yake:

“Maisha huku yamekuwa magumu kutokana na virusi hivi vya korona. Mimi kwa bahati nzuri naendelea kwenda kazini na kurudi nyumbani, lakini mke na watoto wangu wamefungiwa nyumbani. Shule zilifungwa.

“Tunaruhusiwa kutoka nyumbani kwa shughuli tatu pekee – kazi, kununua chakula ama kununua dawa. Maduka mengi na mikahawa na shughuli nyingi za kibiashara zilifungwa. Maduka ya ‘supermarket’ yanauza tu chakula. Huwezi kununua nguo. Huwezi kununua bidhaa nyingine isipokuwa chakula na dawa.

“Watu wanakaa nyumbani. Jua tunalionea tu kwa ‘balcony’. Tunatazama runinga na kujaribu kupitisha muda kwa kucheza na watoto. Siku ni ndefu sana. Hakuna mahali pa kwenda.

“Hata ‘supermarket’ yenyewe ukienda hautapendezwa na picha utakayokumbana nayo. Wateja wote wanavaa ‘masks’ na glavu.

“Tunafaa kukaa umbali wa mita moja baina ya watu. Kuna wingu la hofu. Mimi niko mji wa Verona katika eneo la Veneto. Nimekuwa hapa kwa miaka kumi. Sijawahi ona mambo kama haya.

“Bei ya bidhaa haijapanda. Lakini kama vile ni sharti tukae nyumbani, lazima tunakula zaidi kuliko awali. Lakini vyakula viko kwenye maduka kama mbeleni.

“Hakuna anayeng’ang’ania. Hakuna foleni. Tunatumai hali ya kawaida itarejea ili tuendelee na maisha yetu bila balaa kubwa, ambayo virusi hivi imetusababishia. “