HabariSiasa

CORONA: Mola twakuomba utusamehe – Uhuru

March 18th, 2020 1 min read

Na BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta ametenga Jumamosi ijayo kuwa siku ya kuomba Mungu alinde Kenya kutokana na janga la corona.

Kwenye tangazo rasmi, Rais Kenyatta alisema corona ni tisho kwa ulimwengu na ingawa serikali yake imechukua hatua za kukabili kuenea kwa virusi hivyo, kuna haja ya kumgeukia Mungu.

“Hata kama tumeweka juhudi hizi, hatuwezi kupuuza haja ya kumgeukia Mungu. Katika hali kama hizi, kama vile tulivyofanya awali katika nchi yetu, huwa tunamgeukia Mungu kwanza kushukuru kwa baraka tele na pia kumgeukia kueleza hofu yetu na kutafuta mwongozo na ulinzi wake,” alisema Rais Kenyatta.

Alisema Wakenya wanatambua bila Mungu hawawezi chochote na kwamba, alifikia uamuzi wa kutenga siku ya maombi baada ya kushauriana na Wakenya wa kawaida na viongozi wa kidini.

“Tutamuomba Mungu atusamehe kwa makosa tunayoweza kuwa tulimtendelea,” Rais alisema.

Wakenya wataomba wakiwa nyumbani, maeneo ya kazi ili kuepuka kukusanyika kufuatia agizo la serikali ya kupiga marufuku mikutano ya watu wengi.