Habari Mseto

CORONA: Mtindo ni malipo ya dijitali kama Bitcoin

March 16th, 2020 1 min read

Na Mishi Gongo

BAADHI ya wafanyabiashara Mombasa wameanza kupendekezea wateja wao wafanye malipo kupitia simu za mkononi ili kupunguza uwezekano wa kuambukizana virusi vya corona.

“Nimeamua kutumia njia hii ya malipo ili kupunguza mgusano kati ya wateja wangu na wahudumu, hakuna ajuwae pesa zimeshikwa na watu wangapi, hivyo kubadilishana pesa pia kunawaweka watu kwenye hatari ya kuambukizana,” akasema Bw Willies Kamau anayemiliki duka la jumla katika eneo la VOK eneo bunge la Nyali.

Wateja walieleza kuridhishwa na hatua hiyo wakisema serikali inafaa kusisitiza malipo kwa njia ya simu na sarafu za dijitali kama Bitcoin ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huo.

Bi Jackline Mutisya, mteja katika duka hilo alisema Wakenya wanapaswa kukumbatia kila njia itakayopunguza hatari ya kusambaa kwa virusi hivyo.

Alitaja malipo kwa njia ya simu ni moja wapo ya tahadhari za kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo.

Muuzaji mwengine, Bi Margaret Isumbi alisema japo bado anapokea pesa kwa wateja wake anapendekeza malipo kupitia simu ya rununu.