Habari Mseto

CORONA: Mvutano ufuoni polisi wakikataza wakazi kuogelea

March 16th, 2020 1 min read

MISHI GONGO na WINNIE ATIENO

KIZAAZAA kilizuka jana katika fuo za Bahari Hindi wakati polisi walipojaribu kuzuia waogeleaji kuingia majini kujivinjari ilivyo desturi yao kila wikendi.

Hatua ya polisi ilikuwa imetokana na vile serikali ilitahadharisha wakazi kuepuka sehemu za msongamano kama njia mojawapo ya kudhibiti virusi vya corona kuenea.

Wakazi walijitetea vikali wakidai maji ya chumvi huwa ni tiba, na hatimaye polisi wakawaruhusu kwenda kuogelea.

“Maji ya bahari yana uwezo wa kujisafisha yenyewe. Maji haya pia ni tiba ambayo ilitumika na wazee wetu kutubu magonjwa mbalimbali,” akadai Bw Charo Mzungu, ambaye ni mfanyabiashara ufuoni Jomo Kenyatta.

Katika kiingilio cha ufuo huo, muungano wa wafanyabiashara waliwapa waliozuru bahari hiyo maji na sabuni kama njia mojawapo ya kudhibiti ugonjwa huo.

Bw Joseph Nenge, mwanachama wa muungano huo alisema walichukua hatua hiyo hapo jana, kufuatia kupatikana visa vya walioambukizwa virusi hivyo nchini.

Mfanyabiashara mwingine Bw Fredrick Kambi alisema hatua hiyo inakumbwa na changamoto kufuatia eneo hilo kuwa na viingilio zaidi ya kimoja. Aidha alisema wanahofia kudorora kwa biashara zao iwapo serikali itaamua kuweka marufuku kwa wakazi kuzuru eneo hilo.

Jumamosi usiku, wakazi wengi wa Mombasa walifurika katika vilabu vya Mtwapa kaunti ya Kilifi baada ya Kaunti ya Mombasa kuagiza vilabu eneo hilo vifungwe.

Klabu maarufu ya Danka eneo la Mtwapa ilifurika huku Casablanca iliyoko mjini Mombasa ikikosa wateja huku makahaba wakilalamikia kudorora kwa biashara.

“Hatuelewi ni kwa nini kaunti iamue kuchukua hatua hii, tunategemea biashara ya klabu kulisha familia zetu,” akasema Bi Joyce.