Habari Mseto

CORONA: Mwanahabari aliyetamani kuzuru Kenya

April 8th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

Tanzania ni mojawapo ya mataifa yaliyochukua hatua za haraka kupunguza uwezekano wa maambukizi ya virusi hatari vya corona kupitia kusalimiana kwa mikono kwa kuvumbua salamu ya aina yake ya kutumia miguu.

Majirani hao wa Kenya wamethibitisha visa 24 na kifo kimoja tangu mkurupuko wa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19 kuanzia nchini Uchina zaidi ya miezi mitatu iliyopita na kusambaa katika zaidi ya mataifa 200.

Mwandishi huyu alizungumza na Mkenya Victor Abuso, ambaye ameishi jijini Dar es Salaam kwa miaka 10 sasa, kutaka kujua hali ilivyo nchini Tanzania humo. Mwanahabari huyo alizungumzia masuala mengi tu kuhusu maambukizi ya virusi vya corona ikiwemo salamu za kutumia miguu alizoanzisha Rais John Pombe Magufuli kama mojawapo ya njia za kuzuia uenezaji wa virusi hivyo.

“Kabla ya maambukizi haya ya virusi vya corona, hakuna aliyejali chochote hapa Dar es Salaam. Mikusanyiko mikubwa sokoni kama Kariakoo iliendelea kushuhudiwa kama kawaida.

Kwenye vyombo vya usafiri kama daladala, abiria waliendelea kubanana bila kujali athari zinazoweza kutokea.

Wasiwasi ulianza kujitokeza pale tuliposikia kuwa maambukizi yameripotiwa nchini Kenya, hapo serikali ikaanza kuchukua hatua na kuwaambia wananchi kuchukua tahadhari ya kuepuka mikusanyiko, kunawa mikono kwa maji na sabuni na kutumia kemikali za kutakasa mikono.

Maambukizi haya kwa sasa nchini Tanzania si kama ilivyo huko nyumbani nchini Kenya. Mimi ambaye nilitamani kuja Kenya lakini siwezi, sifahamu hali hii itaisha lini.

Salamu ambayo ilianzishwa na Rais Magufuli alipokutana na mwanasiasa wa uoinzani Maalum Sharif Hamad katika Ikulu Dar es Salaam, nafikiri alikuwa anatuma ujumbe kuwa kila mmoja wetu nchini Tanzania achukue tahadhari. Wananchi waache kusalimiana ili kuzuia uenezaji. Alipofanya hivyo, imekuwa salamu maarufu sasa.

Naishi na familia mjini hapa. Katika muda wa ziada, mimi hutumika kanisani. Mimi ni mwimbaji kwenye Kwaya ya Vijana ya Kanisa Anglikana, Ilala Dar es Salaam. Mimi pia hupenda kutembea, kupata upepo katika fukwe mbalimbali.

Namwomba Mungu atunusuru na hili janga.”