Habari Mseto

Corona na ICC zimemtoa pumzi Ruto – Wadadisi

November 9th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya Naibu Rais William Ruto ya kusitisha mikutano yake ya kisiasa, imeibua hofu kwamba ameingiza baridi kufuatia matukio ya hivi majuzi ikiwa ni pamoja na hofu ya kufufuliwa kwa kesi iliyomkabili katika Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC).

Mnamo Jumanne wiki jana, Dkt Ruto alitangaza kuwa amefuta mikutano ya kampeni yake ya kusaidia walala hoi kufuatia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini.

“Kuongezeka kwa maambukizi ya corona kuna hatari ya kuzuka kwa mkumbo wa pili wa msambao wa virusi hivyo. Kwa sababu hii, nimeamua kusitisha hafla zangu za umma hadi nitakapotangaza,” Dkt Ruto alisema.

Tangazo hilo lilijiri siku moja baada ya ICC kutangaza kuwa wakili Paul Gicheru aliyekuwa akisakwa kwa miaka mitano kwa madai ya kuhonga mashahidi wa kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 dhidi ya Ruto kujisalimisha.

Ingawa Dkt Ruto alisema kwamba aliahirisha mikutano yake aliyopanga Makueni, Machakos na Kitui kufuatia ongezeko la maambukizi ya corona, maswali yameibuka kuhusu sadfa ya hatua hiyo na kujisalimisha kwa Bw Gicheru huko ICC.

Kuna wasiwasi kwamba kujisalimisha kwa wakili huyo ICC ambako hakukutarajiwa, kunaweza kuvuruga azima ya Dkt Ruto ya kugombea urais 2022.Mnamo Jumatano, ICC ilitangaza kuwa kesi ya Bw Gicheru itaanza mara moja hatua ambayo wadadisi wanasema huenda imemfanya Dkt Ruto kutokwa na pumzi.

“Hii ndiyo sababu ya kusitisha mikutano ya kisiasa. Anataka kujipanga upya,” Ike Kenneth Ojuok alisema kwenye Twitter kujibu taarifa ya Dkt Ruto.

Wakili huyo alifikishwa mahakamani Ijumaa kutambuliwa ambapo alisema hakushurutishwa na yeyote kujisalimisha.Ikizingatiwa kwamba amekuwa akikaidi marufuku ya wizara ya afya kuhusu mikutano ya hadhara, wachanganuzi wanasema kwamba huenda amegundua kwamba atalaumiwa kwa maambukizi ya corona yanayoongezeka kwa viwango vikubwa katika kaunti.

Baadhi ya Wakenya wanasema kwamba ikizingatiwa ugonjwa huo umeanza kusambaa na kuua watu wengi mashuhuri, huenda Dkt Ruto anahisi kwamba anaweka afya yake hatarini kwa kuandaa mikutano hiyo.

Watu wamekuwa wakisongamana katika mikutano anayoandaa wakiwa hawajavalia barakoa, ikiwa ni kukiuka kanuni za wizara ya afya za kuzuia msambao wa corona.

Mwezi jana, kamati ya kitaifa ya ushauri wa usalama (NSAC) ilipopiga marufuku mikutano yake kaunti za Nyamira, Kakamega na Muranga, Dkt Ruto na wandani wake walilalamika vikali.Kamati hiyo ilitaja ukiukaji wa kanuni za kuzuia corona kama sababu ya kuharamisha mikutano ya kisiasa nchini.

Kulingana kanuni za baraza hilo, mikutano ya kisiasa inafaa kuidhinishwa na wakuu wa vituo vya polisi inakoandaliwa.Baada ya Dkt Ruto na wandani wake kuteta kwamba ndio walilengwa na kanuni hizo, waliruhusiwa kuendelea na mikutano.

“Inashangaza anaweza kusitisha mikutano ambayo alilaumu maafisa wa serikali kwa kutumia polisi kuisimamisha kana kwamba hakukuwa na corona nchini wakati alipolalamika. Kuna sababu kuu kuliko ongezeko la corona na ninahisi inatokana na hofu fulani,” asema mdadisi wa siasa Geff Kamwanah.

Duru zinasema kuwa Dkt Ruto amechanganyikiwa baada ya juhudi zake za kutaka mdahalo kuhusu mapendekezo ya ripoti ya maridhiano kuzimwa.

Mchanganuzi wa masuala ya siasa Herman Manyora anasema kwamba Dkt Ruto ameingiwa na baridi baada ya kugundua kuwa mbinu zake za kupinga BBI hazifaulu.

Kwa kusitisha mikutano ambayo amekuwa akitetea hata mbele ya rais, wachanganuzi wanasema kwamba huenda Dkt Ruto ametambua ni hatari kushindana na rais aliye mamlakani.