Habari

CORONA: Nauli yapanda

March 22nd, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WAMILIKI na wahudumu wa matatu jana walianza kupandisha nauli, siku moja tu baada ya kuagizwa na serikali wapunguze idadi ya abiria kama njia ya kukabili maambukizi ya virusi vya corona.

Katika miji ya Nyeri na Nakuru, wenye matatu walipandisha nauli kwa kati ya asilimia 50 na mia moja.

Matatu za Nyeri kuekelea Nairobi ziliongeza nauli kutoka Sh300 hadi Sh600 huku wale wanaolekea Nanyuki kutoka mji huo wakilipa Sh350 kutoka Sh150.

Waliokuwa wakisafiri kutoka Nyeri hadi Nyahururu na Nakuru walikuwa wakitozwa nauli ya Sh500 na Sh600 mtawalia.

“Tunafaa kubeba huu mzigo sisi sote ili biashara zetu zisiathirike. Hata hivyo, serikali inafaa kupunguza gharama ili abiria wasiumie sana,” akasema mwenyekiti wa chama cha matatu cha 2NK, Bw James Kahiro.

Mjini Nakuru, hali ilikuwa kama Nyeri. Nauli ilipandishwa kwa wasafiri waliokuwa wakielekea jijini Nairobi.

Kwa kawaida abiria hao hulipa kati ya Sh300 na Sh400 lakini jana ilipanda hadi Sh600.

Dereva mmoja kwa jina Paul Waithaka, alisema kuwa, hawakuwa na jingine ila kuongeza nauli kwa sababu gharama ya biashara ya uchukuzi ni ya juu mno.

Hata hivyo, matatu ya kubeba abiria 14 zinazotoka Eldoret hadi Nakuru zilipuuza agizo la kubeba abiria wanane na zinaendelea kubeba idadi ya abiria kama kawaida. Walisema wakuu wa vyama vyao hawajawapa mwelekeo wa kubeba abiria wachache.

Mnamo Ijumaa, Waziri wa Afya Bw Mutahi Kagwe aliamuru kuwa matatu inayobeba abiria 14 ibebe wanane. Zile za abiria 25 zinatakiwa zibebe abiria 15 pekee.

Hata hivyo, wadau katika sekta ya uchukuzi wanasema iwapo ni sharti watimize agizo hilo, serikali yapaswa kupunguza bei ya mafuta ili kufidia hasara watakayopata kwa kuwabeba abiria wachache kuliko kawaida.

Naibu mwenyekiti wa Muungano wa Kitaifa wa Wamiliki wa matatu Nchini (MOA), Bw Salim Batesi, alisema wapo tayari kutekeleza mikakati yote ya usafi iliyowekwa lakini pia lazima wadhibiti biashara zao zisiangamie kutokana na hasara.

“Kupunguza idadi ya abiria ni sawa kwetu lakini kwa sasa tunapata hasara kubwa. Tungependa serikali ipunguze bei ya mafuta na iwapo hilo halitafanyika, basi abiria tunaowabeba watalipa nauli ya juu kugharimia mahitaji yetu,” akasema Bw Batesi.

Mwenyekiti wa muungano huo Benson Mkune naye alisema kuripotiwa kwa virusi vya corona nchini kumeathiri sekta ya uchukuzi kimapato.

“Katika sekta ya matatu, sisi hulipia bima, maegesho, mafuta, dereva na utingo. Iwapo serikali itapunguza bei ya mafuta, basi hatutaongeza nauli na kuwaumiza wasafiri,” akasema Bw Nkune.

Mshirikishi wa wamiliki wa matatu Pwani, Bw Salim Mbarak, alisema matatu zote zimekuwa zikitimiza viwango vyote vya usafi vinavyohitajika akitoa mfano wa abiria kunawa mikono kwa kutumia dawa ya kuua viini kabla ya kuingia garini.

“Sharti biashara iwe na faida. Ikiwa mapato yako yatapungua, sharti ibuni njia za kuziba pengo hilo. Kwa hivyo, tutakoma tu kupandisha nauli ikiwa serikali itatupa mafuta bure au kwa bei iliyopunguzwa,” akasema mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA) Simon Kimutai.

 

Ripoti za WACHIRA MWANGI, PHYLIS MUSASIA na NICHOLAS KOMU