Kimataifa

Corona ni shetani, dawa ni kwenda kanisani, msikitini – Magufuli

March 24th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

RAIS John Magufuli amesema Tanzania haitafunga maeneo ya ibada akisisitiza virusi vya corona haviwezi kushinda nguvu za Mungu.

Alisema haya akiwa kanisani mnamo Jumapili mjini Dodoma, muda mfupi tu kabla ya kutangaza kwamba visa sita zaidi vilikuwa vimethibitishwa.

Hii ilifikisha idadi ya maambukizi nchini humo hadi 12.Magufuli kwenye hotuba yake alitaja virusi hivyo kama “shetani.”

“Hatufungi sehemu za ibada. Huko ndiko kuna uponyaji wa kweli. Corona ni shetani na hawezi kuishi katika mwili wa Yesu,” akawaambia waumini waliomshangilia.H

ata hivyo, Magufuli alikashifiwa vikali kwa kuwataka watu kuendelea kwenda sehemu za ibada wakati huu ambapo masharti makali yanapaswa kutekelezwa kuzuia mkurupuko wa virusi vya corona.

Mwanasiasa wa upinzani Zitto Kabwe alikosoa matamshi ya Magufuli na kumhimiza kufunga misikiti na makanisa ili kuimarisha juhudi za kudhibiti ugonjwa huo.

“Tusibishane na sayansi. Virusi vya corona ni vibaya sana,” alisema KabweMnamo Jumamosi, mwanachama wa kamati kuu ya chama cha upinzani cha Chadema, Lazaro Nyalandu, alitoa wito kwa serikali kupiga marufuku mikutano yote ya hadhara na kufunga mipaka.