Habari Mseto

CORONA: Onyo baadhi ya dawa zikitumika bila ushauri wa wataalamu zinasababisha upofu

March 27th, 2020 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

BODI ya Dawa na Sumu imeonya kwamba matumizi ya dawa za Chloroquine na Hydroxychloroquine yanaweza yakasababisha upofu iwapo zinatumika bila ushauri wa daktari au mtaalamu wa afya.

Hii ni kufuatia habari kwamba baadhi ya watu sasa wanafurika katika maduka ya dawa kununua dawa hizi zinazosemekana kutibu ugonjwa wa corona.

Kulingana na bodi hiyo, utafiti wa iwapo dawa hizo zinaweza kuponya ugonjwa wa Covid-19 bado unaendelea na hakuna thibitisho kwamba zinaweza kuponya.

“Bodi hii imekataza uuzaji wa dawa hizi kwa yeyote ambaye hana maagizo maalum kutoka kwa daktari,” ikasema bodi hiyo kwenye taarifa.

Bodi hiyo imeongeza kuwa kuna wagonjwa ambao hutegemea dawa hizi katika maisha yao ya kila siku kutokana na maradhi mbalimbali na ni wao tu wanaruhusiwa kuzitumia.

Bodi imeonya kuwa watakaokiuka sheria na kuuza dawa hizi kwa njia isiyopfaa, watachukuliwa hatua kali.