Corona: Onyo kuhusiana na utoaji chanjo kwa halaiki

Corona: Onyo kuhusiana na utoaji chanjo kwa halaiki

Na MASHIRIKA

UWEZO wa kinga ya pamoja kutumika katika kuzuia maambukizi ya Covid-19 umezidi kujitokeza kama jambo lisilowezekana, kwa mujibu wa wanasaysansi.

Kupokea chanjo au kuambukizwa virusi vya corona hakuwezeshi kinga ‘kamili’ ya mwili hivyo kumaanisha kwamba wanaobeba virusi (carriers) bado wanaweza kusambaza virusi hivyo.

Kinga ya pamoja (herd immunity) hufanikishwa wakati watu katika jamii wana kinga imara ya mwili dhidi ya virusi au bakteria zinazosababisha maradhi,hivyo basi kumaanisha kwamba hawawezi kuambukizwa wala kusambaza.

Mataifa ya ulimwengu yapo mbioni kufikia kiwango kinachohitajika kwa sababu hatua hiyo itapunguza viwango vya maambukizi na kusaidia maisha kurejelea hali ya kawaida.

Hata hivyo, wanasayansi wameonya kwamba kuna masuala kadhaa yanayozuia kufanikisha lengo hilo.

Huku utafiti wa kina ukithibitisha kwamba chanjo hupunguza uwezekano wa watu kufa au kulazwa hospitalini, watu waliopokea dozi kamili za chanjo bado wanaweza kusambaza virusi vya corona.

Wanasayansi hata hivyo wamesema kwamba, jambo hilo linafanya iwe muhimu hata zaidi kupokea chanjo kwa sababu viwango vya juu zaidi vya kinga ya mwili katika jamii, vitapunguza kusambaa kwa Covid-19.

Wamefafanua kuwa chanjo zitalinda maelfu ya watu wanaokabiliwa na hatari zaidi dhidi ya kufa kutokana na mikurupuko mipya katika siku za usoni.

Dkt Alexander Corbishley, mtafiti kuhusu afya ya umma katika Chuo Kikuu cha Edinburgh alisema kuwa ‘Chanjo zinachangia pakubwa kupunguza makali ya Covid-19 hivyo kumaanisha kuwa zinaokoa maisha.

“Chanjo huwa hazizuii kila mtu dhidi ya kuambukizwa na kusambaza ugonjwa huo kwa mtu mwingine. Virusi hivyo bado vinaweza kuzunguka katika jamii, licha ya viwango vya juu vya chanjo au maambukizi ya awali.”

“Hivyo basi tunapaswa kuwapa chanjo watu wengi zaidi iwezekanavyo na kukubali kwamba Covid-19 itaendelea kusambaa katika jamii,” alisema.

Dhana ya kinga ya pamoja iliangaziwa kwa mara ya kwanza mnamo Machi mwaka uliopita, wakati virusi vya corona na usambazaji wake vilikuwa bado havieleweki.

Mshauri mkuu wa wanasayansi Sir Patrick Vallance alidai kuwa kiwango kinachofaa kinaweza kutimizwa ikiwa karibu asilimia 60 ya taifa au watu milioni 40 wana kiwango fulani cha kinga.

Kauli yake ilizua utata mkubwa huku serikali, ambayo haikuwa na chanjo zozote za kuokoa maisha wakati huo, ikishutumiwa dhidi ya kupanga njama za kuwaacha maelfu ya watu kuaga dunia ili kutimiza kiwango hicho.

You can share this post!

Lukaku pua na mdomo kurudi Chelsea

Messi aagana na Barcelona kwa huzuni na machozi