Michezo

CORONA: Pep Guardiola afanya hisani

March 26th, 2020 3 min read

Na MASHIRIKA

BARCELONA, UHISPANIA

KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City ametoa msaada wa Sh129 milioni ili kusadia waathiriwa wa virusi vya corona nchini Uhispania.

Baada ya Italia, Uhispania ndilo taifa la pili ambalo limeathiriwa pakubwa zaidi na janga na corona barani Ulaya.

Kufikia jana, ugonjwa huo ulikuwa umewaathiri zaidi ya watu 440,000 huku zaidi ya vifo 20,000 vikiripotiwa kutokea duniani kote.

Mchango wa Guardiola uliwekwa katika hazina ya chuo kimoja cha matibabu jijini Barcelona na Wakfu wa Angel Soler Daniel ambao pia umethibitisha kupokea mchango wa Sh108 milioni kutoka kwa nyota Lionel Messi.

Mnamo Jumanne, takwimu zilionyesha kwamba zaidi ya watu 3,400 walikuwa wameaga dunia nchini Uhispania kutokana na corona huku takriban watu 41,000 wakiambukizwa virusi vya gonjwa hilo linalozidi kutisha ulimwengu mzima.

Pesa ambazo zinazidi kutolewa na wanamichezo mbalimbali kukabiliana na corona katika mataifa tofauti zinalenga kununua vifaa vya afya kwa wagonjwa na wahudumu wa afya hospitalini.

Jimbo la Catalonia nchini Uhispania ndilo lililoathiriwa pakubwa na janga la corona.

Zaidi ya asilimia 50 ya waathiriwa wote nchini Uhispania wanatokea katika eneo hilo ambalo ni makao makuu ya klabu ya Barcelona.

Wiki jana, Messi alitoa mchango wa Sh112 milioni nyinginezo kwa hospitali mbili katika nchi ya Argentina alikozaliwa.

Siku chache baada ya wito kutolewa kwa klabu, mashirika na wachezaji maarufu wanaopokea mishahara minono katika fani mbalimbali za spoti kuchangia sehemu ya mabilioni yao kupiga jeki vita vya kudhibiti ueneaji wa virusi vya corona, baadhi yao wanazidi kuitikia.

Nyota wa zamani wa Manchester United, Gary Neville aliyetoa vitanda 176 katika hoteli ya Hotel Football jijini Manchester, London alikuwa wa hivi karibuni kuwataka wanasoka wa haiba kubwa kote duniani kuonyesha ukarimu wao na kujitokeza kukabiliana na janga hilo.

Fowadi Robert Lewandowski wa Bayern Munich pamoja na mkewe Anna tayari wametoa Sh129 milioni huku Leon Goretzka na Joshua Kimmich ambao ni wachezaji wengine wa Bayern wakichangia Sh115 milioni katika hazina ya ‘We Kick Corona’ waliyoianzisha wiki iliyopita.

Leroy Sane wa Manchester City pia alichangia Sh1 milioni katika hazina hiyo itakayoshuhudia wachezaji wote wa Borussia Monchengladbach wakichangia nusu ya mishahara yao ya kila wiki.

Mwanzoni mwa wiki jana, kiungo matata wa Man-United, Paul Pogba alianzisha mpango wa kuchangisha pesa za kupiga jeki juhudi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) kukabiliana na corona.

Mzawa huyo wa Ufaransa aliasisi mradi huo akiadhimisha miaka 27 ya kuzaliwa kwake.

Alitoa nusu ya Sh3.8 milioni anazolenga kuchangisha kila siku kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Kwa upande wake, nyota Cristiano Ronaldo wa Juventus alitoa hoteli zake nne katika miji ya Funchal na Lisbon, Ureno kuwa vituo vya afya na kliniki za kuhudumia waathiriwa wa corona nchini humo.

Siku chache baadaye, mshambuliaji Marcus Rashford wa Man-United alitoa kiasi kisichojulikana cha pesa kwa minajili ya chakula cha watoto katika maeneo mbalimbali jijini London, Uingereza.

Awali, vikosi vya Aston Villa, Watford na Brighton vililazimika kutoa chakula cha wachezaji wao kwa mayatima, maafisa wa afya na raia maskini nchini Uingereza baada ya kuahirishwa kwa mechi zote za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) hadi Aprili 30.

Hadi kuahirishwa upya kwa kipute hicho kilichotazamiwa awali kurejelewa Aprili 3, vyakula vingi kwa minajili ya wachezaji, wasimamizi na mashabiki wa klabu hizo vilikuwa vimeandaliwa katika vituo mbalimbali jijini London.

Vinara wa Villa na Brighton wamepania kuhakikisha kwamba vyakula hivyo haviharibiki bure, na badala yake vinawaendea wasiojiweza; hatua sawa na iliyochukuliwa na kikosi cha Fulham ambacho kwa sasa kinashiriki Ligi ya Daraja ya Kwanza baada ya kuteremshwa ngazi msimu jana.

Klabu za Villa na Fulham zimetoa chakula kwa zaidi ya familia 1,350 zisizojiweza viungani mwa jiji la London huku Brighton ikitoa matunda, mboga na bidhaa za maziwa kwa maskini katika eneo la Sussex, Uingereza.

Sawa na Man-United, West Bromwich Albion pia wamethibitisha kwamba watawalipa vibarua wao wote mishahara yao licha ya kuongezeka kwa visa vya waathiriwa wa homa kali ya corona. Hatua hiyo ya vikosi hivi imepongezwa sana na watumiaji mbalimbali wa mitandao ya kijamii duniani kote.