CORONA: Pigo kwa wafungwa kesi zikisitishwa
Na Wanderi Kamau
IDARA ya Mahakama imesimamisha vikao vya kusikiliza kesi za kawaida ambazo si za jinai kwa muda wa wiki mbili, ili kudhibiti maenezi ya virusi vya corona nchini kuanzia Jumatatu.
Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, Jaji Mkuu David Maraga alisema kuwa ni kesi za dharura pekee ama zile zenye uzito mkubwa ambazo zitasikizwa.
Vile vile, aliwashauri polisi kutatua kesi mpya zitakazoibuka katika vituo vyao, kulingana na kanuni ambazo zilitolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi Hilary Mutyambai.
Katika muda huo, washukiwa na watu wanaozuiliwa katika rumande hawatafikishwa mahakamani ili kesi zao kutajwa.
Kesi za kutoa hukumu pia hazitasikizwa huku vikao vya wazi vya mahakama pia vikisimamishwa.
Bw Maraga alisema kuwa mikakati hiyo inalingana na tahadhari ambazo zimetolewa na Serikali ya Kitaifa kudhibiti shughuli mbalimbali za umma nchini.
Alisema kuwa idara hiyo imebuni kamati maalum, ambayo itakuwa ikishauriana na Kamati ya Kitaifa ya Dharura Kukabili Maenezi ya Corona iliyobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta mwezi uliopita.