Michezo

'Corona sasa haipo EPL'

June 12th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

HAKUNA kisa chochote cha maambukizi mapya ya virusi vya corona kilichopatikana miongoni mwa washikadau wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya jumla ya watu 1,195 kupimwa.

Raundi ya sita ya vipimo vya afya miongoni mwa wafanyakazi, vibarua, marefa, wachezaji na maafisa wa vikosi vyote 20 vya EPL ilifanywa kati ya Juni 4-5, 2020 na matokeo kutolewa jana.

Mtu mmoja alipatikana na virusi vya homa kali ya corona mwishoni mwa vipimo vya raundi ya tano na hivyo kufikisha idadi ya maambukizi kuwa 13 hadi sasa.

Kipute cha EPL ambacho kilisitishwa kwa muda tangu Machi 13 kitarejelewa Juni 17 bila mahudhurio ya mashabiki viwanjani. Aston Villa na Sheffield United watavaana ugani Villa Park kabla ya Manchester City kuialika Arsenal ugani Etihad.

Mechi hizo ni zile zilizokuwa zimesalia kwa vikosi hivyo kucheza ili kufikia idadi ya michuano 29 ambayo wapinzani wote wengine 16 walikuwa wamepiga hadi kipute hicho kiliposimamishwa kwa muda kutokana na janga la corona mnamo Machi 13.

Mechi zote za raundi nzima ya 30 zimeratibiwa kusakatwa kati ya Ijumaa ya Juni 19 na Jumapili ya Juni 21, 2020.

Hadi sasa, Liverpool wanaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 25 zaidi ya nambari mbili Man-City huku Bournemouth, Villa na Norwich City wakining’inia padogo mkiani kwa pointi 27, 25 na 21 mtawalia.