Habari Mseto

CORONA: Serikali inunulie raia viyeyushi – Wetang'ula

March 16th, 2020 1 min read

Na Charles Lwanga

SENETA wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula ameitaka serikali igharamie dawa za kuua viini zinazotumiwa kudhibiti uenezaji wa virusi vya corona.

Maeneo mengi ambako watu hujumuika ikiwemo makanisa, mikahawa na matatu kadhaa zimeanza kutoa huduma za kusafisha mikono kutumia dawa hiyo maalum kukabili virusi hivyo.

Akizungumza jana katika kanisa la Malindi Pefa alipohudhuria harambee, kinara huyo wa chama cha Ford Kenya pia aliwahimiza viongozi wa kidini kuombea nchi pamoja na ulimwengu mzima kutokana na virusi hivyo.

“Ugonjwa huu ni wa kushangaza. Mara nyingi mlipuko wa namna hii kama vile Ebola huambukiza watu maskini lakini cha ajabu, huu ugonjwa unaathiri hata matajiri,” alisema.

Aliongeza, “Lakini hamfai kuwa na wasiwasi kwa sababu si hatari sana kama milipuko mingine. Tunafaa tunawe mikono yetu jinsi maafisa wa afya wametuhimiza kuzuia uambukizaji.”

Wakati huo huo, Bw Wetang’ula aliitaka serikali itenge fedha za kuinua sekta ya utalii kutokana na madhara ya corona.