CORONA: Shule bado kujiandaa

CORONA: Shule bado kujiandaa

WANDERI KAMAU na FAITH NYAMAI

HUKU shule zikitarajiwa kufunguliwa Jumatatu ijayo, hofu imeibuka nchini kuhusu hali na mazingira ya shule za umma ikiwemo uhaba wa madarasa na walimu katika kipindi hiki cha janga la corona.

Walimu wakuu wanasema hawajui wanafunzi watakakosomea baada ya miundomsingi katika shule nyingi kuharibika kwa kutotumiwa kwa karibu miezi kumi tangu shule zilipofungwa katika juhudi za kukabili maambukizi ya Covid-19.

Licha ya kutangaza shule zitafunguliwa wiki ijayo kwa kuzingatia kanuni za kuzuia corona, serikali haijafanikisha ujenzi wa madarasa mapya ili kuzuia misongamano ya wanafunzi.

Hofu hiyo pia inahusu usalama wa wanafunzi kiafya, kwani shule nyingi bado hazijabuni mikakati thabiti kuhakikisha wanafunzi watazingatia kanuni ambazo zimetolewa na Wizara ya Afya kuhusu maambukizi ya virusi vya corona.

Hali hiyo imezua wasiwasi miongoni mwa wazazi, ambapo wengi wameeleza kutoridhishwa na mikakati ambayo serikali imechukua kutayarisha shule kukabili hali hiyo mpya.

Hilo linajiri huku maafisa wa elimu katika vitengo mbalimbali wakiendelea na harakati za mwisho mwisho kuhakikisha wanafunzi wote wamerejea shuleni.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, wadau wengi wa elimu, miongoni mwao wazazi, walieleza kutoridhishwa na hali ilivyo katika shule nyingi.

“Inasikitisha kuwa serikali inasisitiza kuhusu haja ya wanafunzi kurejea shuleni wakati shule zenyewe ziko katika hali mbaya kimiundomsingi. Baadhi ya madarasa yameharibika. Madirisha hayapo kati ya matatizo mengine. Haya ni mambo yanayopaswa kushughulikiwa kabla ya wanafunzi kurejea,” akasema mzazi ambaye hakutaka kutajwa.

Walimu wakuu wa shule kadhaa walisema shule nyingi hazina madarasa ya kutosha kuhakikisha wanafunzi hawasongamani kwa mujibu wa kanuni ambazo zimetolewa na serikali.

Vile vile, imekuwa vigumu kwa shule nyingi, hasa zilizo katika maeneo ya mashambani na mitaa ya mabanda, kupata maji ya kutosha kuhakikisha wanafunzi wananawa mikono kila mara.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo jana, Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA), Bw Nicholas Maiyo, alisema wanafahamu kuhusu changamoto hizo, ijapokuwa wazazi wanafaa kushirikiana na serikali katika kutatua hali hiyo.

“Huu umekuwa mwaka mgumu kwetu sisi sote. Hivyo, ni muhimu wadau wote kushirikiana badala ya kuelekezeana lawama ili kuhakikisha wanafunzi wanarejelea masomo yao licha ya ugumu ambao umekuwepo,” akasema Bw Maiyo.

Hata hivyo, mshirikishi mkuu wa Vuguvugu la Elimu Yetu, Bw Joseph Wasikhongo aliilaumu serikali kwa kutochukua hatua zozote kuimarisha hali za shule kabla ya wanafunzi kurejea.

“Serikali haijachukua hatua za kutosha kuhakikisha mazingira ya wanafunzi ni salama wanaporejelea masomo. Inapaswa kuwa imeweka juhudi zaidi kuliko hali ilivyo sasa,” akasema Bw Wasikhongo.

Mnamo Septemba, Rais Uhuru Kenyatta alizindua mpango wa Sh1.9 bilioni kuziwezesha shule kupata madawati mapya yanayoziungatia kanuni za kukabilki corona.

Serikali pia ilitangaza mpango wa kuziwezesha shule kupata fedha ili kuimarisha miundomsingi yake zinapojitayarisha kuwapokea wanafunzi.

Licha ya ahadi hiyo, walimu wakuu wengi wanasema bado hawajapokea fedha hizo kumaanisha hakuna dawati za kutosha shuleni.Hata kama dawati zingekuwemo, bila madarasa ya kuhakikisha wanafunzi hawakaribiani itakuwa vigumu kuzingatia kanuni za kuzuia corona.

Licha ya malalamishi hayo, Waziri wa Elimu George Magoha amesisitiza kuwa shule zitafunguliwa kama iivyopangwa bila mabadiliko yoyote.Aliwaambia wazazi kuwatayarisha wanao kurejea shuleni, na hawapaswi kutoa visingizio vyovyote kwa kushindwa kuwanunulia vifaa kama vile barakoa.

Hata hivyo alikiri kuwa itakuwa changamoto kuhakikisha wanafunzi hawatangamani wakiwa shuleni.Aliongeza kuwa serikali itatoa usaidizi wa barakoa tu kwa wanafunzi ambao wanatoka katika familia maskini.

Prof Magoha pia aliwaambia wazazi ambao wanao walipata mimba wakati wakiwa nyumbani kuhakikisha wamerejea shuleni. Maelfu ya wasichana katika sehemu mbalimbali nchini walipachikwa mimba baada ya kuwa nyumbani kwa muda mrefu kutokana na janga hilo.

“Ujauzito si ugonjwa. Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha kila mwanafunzi yuko shuleni,” akasema. Idadi ya walimu imepungua ingawa tume ya TSC ilitangaza kuwa itaajiri walimu 5,000 mwaka huu.

You can share this post!

Nauli yapanda Wakenya wakirejea mijini

2020: Corona ilivyozamisha sekta ya elimu