Habari Mseto

Corona: Usimsalimie yeyote kwa mkono kazini, TSC yaonya

March 10th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

TUME ya Huduma kwa Walimu (TSC) imewapiga marufuku wafanyikazi wake kusalimiana kwa mikono katika hatua ya tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Hayo yamejiri Jamhuri ya Demokrasia ya Congo ikithibitisha kisa cha kwanza cha virusi hivyo nchini humo.

Waziri wa Afya wa DRC Dkt Eteni Longondo, alithibitisha kuwa raia wa Ubelgiji alitengwa katika uwanja wa ndege mjini Kinshasa, alipopimwa na kugunduliwa kuwa na virusi hivyo.

Kwenye barua kwa wafanyikazi wa TSC, Mkurugenzi wa Usimamizi Ibrahim Mumin aliwataka wafanyikazi katika makao makuu na ofisi za kaunti wakome kusalimiana kwa mikono, waweke mazingira yao safi na waoshe mikono mara kwa mara.

“Wafanyikazi wanashauriwa kwamba kuanzia leo hadi tutakapowaeleza upya, wanatakiwa wachukue hatua za kujikinga kuambukizwa corona,” alisema kwenye ujumbe huo.

Msemaji wa Serikali, Kanali Mstaafu Cyrus Oguna naye aliruhusu kampuni za simu za Safaricom, Airtel na Telkom ziwatumie wananchi habari za mara kwa mara kuhusu virusi hivyo.

Hayo yalijiri huku Gavana wa Baringo Stanley Kiptis na wahudumu wa afya wakitofautiana kuhusu kuwepo kwa wodi za kuwatenga wagonjwa wa corona.

Japo Bw Kiptis alitangaza kuwa serikali ya kaunti yake imetenga wodi katika hospitali za Eldama Ravine, Marigat, Mogotio na Kabarnet kukabiliana na virusi hivyo, wafanyikazi walisema hakuna wodi yoyote iliyotengwa katika hospitali hizo.

“Madai ya gavana yametushtua. Wodi hizo ziko wapi? Bado hatujaona yoyote? Wafanyikazi wa afya pia hawajapata mafunzo ya kujiandaa kukabili maambukizi kama anavyodai,” alisema mwenyekiti wa chama cha wauguzi tawi la Baringo Elizabeth Yator.

Lakini katika kaunti ya Taita Taveta, afisa mkuu wa Idara ya Afya Bi Philomena Kirote alisema vyumba vitatengwa katika hospitali nne.

“Vyumba hivi haviwezi kuwekwa katika hospitali kubwa kwa kuwa wagonjwa wa Corona hawafai kutangamana na watu. Tutaviweka katika vituo vya afya ambavyo havipati idadi kubwa ya wagonjwa katika kaunti ndogo za Voi, Wundanyi, Mwatate na Taveta,” akasema Bi Kirote.

Serikali za kaunti zilipewa maagizo ya kutenga vyumba hivyo kufikia Machi 15.

Ripoti za Juma Namlola, Flora Koech na Lucy Mkanyika