Habari Mseto

Corona: Viongozi wataka rais azime mikutano, kufunga baa

November 3rd, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

BAADHI ya viongozi wa makanisa na wale wa kisiasa, wanataka Serikali ipige marufuku mikutano yote ya kisiasa, kufunga baa na maeneo ya burudani wakisema imechangia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona nchini.

Jumatatu, idadi ya waliouwa na ugonjwa huo ilifikia 1,027 baada ya watu 14 kufariki ndani ya saa ishirini na nne.

Visa vipya 724 vilithibitishwa ndani ya muda huo kutoka kwa sampuli 5085 zilizopimwa ndani ya muda huo.

Viongozi wa makanisa ya Kievanjelisti wanasema mikutano yote, ikiwemo ya kupigia kampeni ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI), inafaa kusimamishwa mara moja ikiwa maambukizi ya corona yatapungua nchini.

“Hakufai kuwa na mikutano ya kisiasa inayohudhuriwa na maelfu ya watu wakati huu ambao tunalia maambukizi ya corona na vifo vimeongezeka. Tunachoshuhudia ni hatari kwa nchi ambayo ina mfumo dhaifu wa afya,” alisema Askofu Dkt Nicholas Muli ambaye ni mwenyekiti wa EAK, tawi la Machakos.

Dkt Muli alilaumu wanasiasa kwa kuongoza katika ukiukaji wa kanuni za kuzuia kusambaa kwa corona nchini kwa kuandaa mikutano mikubwa ya kisiasa.: Viongozi hao walisema mikutano mikubwa ya kisiasa ambayo imekuwa ikishuhudiwa maeneo tofauti nchini imechangia kusambaa kwa virusi hivyo kwa sababu wanaoihudhuria, wakiwemo viongozi, hawavai barakoa.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga na washirika wao wamekuwa wakiandaa mikutano ya kisiasa kote nchini.

Idadi ya maambukizi ya corona imeendelea kupanda tangu Septemba kafyu ilipolegezwa, vilabu kufunguliwa, ibada makanisani, mazishi na harusi kuruhusiwa.

Dkt Muli alihimiza Rais Kenyatta na Dkt Ruto kuzika tofauti zao za kisiasa ili kutuliza joto la kisiasa linaloendelea kupanda nchini.

Mbunge wa Matungulu, Stephen Mule na mwenzake wa Imenti Kusini, Kathuri Murungi nao wanamuomba Rais Kenyatta kuagiza mikutano ya kisiasa isitishwe ili kudhibiti kusambaa kwa corona.

Bw Mule alisema kuwa mikutano inayoandaliwa na baadhi ya wanasiasa nchini ndio chanzo kikuu cha kusambaza ugonjwa huu,” alisema.

BENSON MATHEKA na GASTONE VALUSI