Habari

CORONA: Visa vyafika 122, mvulana wa miaka 6 afariki

April 3rd, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WATU 12 zaidi wamebainika kuwa na virusi vya corona nchini na kufikisha 122 idadi jumla ya visa vya maambukizi hayo nchini Ijumaa.

Na idadi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa wa Covid-19 unasababishwa na virusi hivyo sasa imeongezeka hadi nne baada ya mtoto wa miaka sita kufariki.

“Nasikitika kuwafahamisha kwamba tumempoteza mgonjwa mwingine kutokana na ugonjwa wa Covid-19. Yeye ni mtoto mvulana mwenye umri wa miaka sita ambaye amekuwa akiugua magonjwa mengine na alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta,” Waziri Msaidizi wa Afya Dkt Mercy Mwangangi akawaambia wanahabari jana katika jumba la Afya, Nairobi

“Wahudumu wa afya ambayo walimhudumia mvulana huyo wametengwa,” akaongeza.

Kaimu Mkurugenzi wa Afya Dkt Patrick Amoth aliongeza kuwa wadi ambako mtoto huyo alilazwa imenyunyizwa dawa ya kuua viini.

“Mvulana huyo alikuwa na dalili zingine za magonjwa ambazo madaktari walikuwa wakishughulikia. Lakini baada ya kufariki sampuli zake zilipatikana na virusi vya corona,” Dkt Amoth akaeleza.

Bi Mwangangi alisema wagonjwa hao wapya ni Wakenya 11 na Msomalia mmoja.

“Saba miongoni mwao wanatoka Nairobi, Kiambu (1), Laikipia (1), Mombasa (2) na Nyeri (1),” akafafanua.