Habari

CORONA: Wadau sekta ya usafiri walia habari za kupotosha mitandaoni zinawaponza

March 5th, 2020 1 min read

Na MAGDALENE WANJA

WAHUDUMU katika sekta ya usafiri wamelalamikia usambazaji wa habari za uongo mitandaoni ambao umewatia hofu wasafiri wanaonuia kuja nchini Kenya.

Kulingana na Chama cha Maajenti wa Usafiri Nchini – Kenya Association of Travel Agents (Kata) – jumbe hizo zimechangia katika kuwapotosha watalii kutoka nchi mbalimbali na hivyo kusababisha hasara kubwa katika sekta hiyo.

“Tunawataka wasafiri wanaonuia kuzuru nchi ya Kenya kuwasiliana moja kwa moja na Kata ili kupata habari za kweli kuhusu hali ilivyo nchini,” amesema mwenyekiti wa Kata Bw Mohammed Wanyoike.

Amesema kuwa sekta ya usafiri wa kimataifa ndiyo imeathirika zaidi na mkurupuko wa virusi vya Corona.

“Tunatarajia viwango vya watalii kwenda chini zaidi hasa wakati nchi nyingi zaidi ulimwenguni zinaendelea kutekeleza marufuku na tahadhari za usafiri kwa raia wake,” akaongeza Bw Wanyoike.

Mwenyekiti wa Kata Bw Mohammed Wanyoike akizungumza kuhusu hasara katika sekta ya usafiri katika kikao na wanahabari jijini Nairobi mnamo Jumatano, Machi 4, 2020. Picha/ Magdalene Wanja

Bw Wanyoike amedokeza kuwa wana matumaini kuwa hali ya kawaida itarejea katika nusu ya pili ya mwaka ambapo wanatarajia wageni wengi kuwasili nchini.

Mwekahazina wa Kata Dkt Joseph Githitu amesema kuwa kutokana na hali hii ngumu ya kiuchumi, mashirika mbalimbali chini ya Kata yanatarajiwa kuwapa wafanyakazi likizo zao za kila mwaka.

“Katika kipindi hiki, hakutakuwa na kazi nyingi kama siku za kawaida na tunashauri kampuni mbalimbali kuchukua nafasi hii kuwapa likizo wafanyakazi ila hatutarajii kuwa kuna wafanyakazi watakaopoteza kazi,” akasema Dkt Githitu.

Waliyasema hayo jana Jumatano walipowahutubia wanahabari.