Habari

CORONA: Wafanyakazi wa mradi wa Lapsset wawekwa kambini kuzuia maambukizi

March 24th, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI imeamrisha wafanyakazi wote zaidi ya 1,000 wanaoendeleza ujenzi wa Bandari Mpya ya Lamu (Lapsset) kuzuiliwa katika kambi yao ya ujenzi iliyoko eneo la Kililana, Kaunti ya Lamu kama njia mojawapo ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, anasema amri hiyo ya wafanyakazi wa Lapsset kuzuiliwa ndani ya kambi tayari imeanza kutekelezwa na kila mfanyakazi anapaswa kuhakikisha ameripoti kambini kabla ya mwisho wa leo Jumanne.

Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kukamilika kwa kikao maalum cha kujadili hali kuhusiana na maradhi ya Covid-19, Bw Macharia alisema hatua ya kuwazuia mahali pamoja wafanyakazi hao ni katika harakati za kuzuia kusiwe na maambukizi ya corona miongoni mwa vibarua, iwe ni wao kuusambaza kutoka nje hadi kwa wenzao walio ndani ya kambi au kutoka ndani ya kambi kusambazwa nje, ikiwemo kwa familia za vibarua hao.

Kamishna huyo pia alisema ziara zote ndani ya kambi ya Lapsset kwa sasa pia ni marufuku hadi pale serikali itakapodhibiti maradhi hayo ya Covid-19 nchini.

Awali serikali ilikuwa imetangaza kwamba haingewafungia ndani wafanyakazi hao na badala yake ikawaamuru wote wanaoishi nje ya kambi kuendelea kuripoti kazini asubuhi na kurudi nyumbani jioni ili kuepuka msongamano kwenye kambi hiyo ya ujenzi wa LAPSSET.

“Awali tulikuwa tumetangaza kwamba wafanyakazi wa Lapsset wasizuiliwe kambini bali wawe wakienda nyumbani kila jioni ili kuepuka msongamano wa watu kambini, lakini tumeafikia kubadili msimamo wetu na sasa hakutakuwa na mtu atakayeruhusiwa kuingia au kutoka kambini baada ya siku ya leo ya Jumanne kukamilika,” amesema Bw Macharia.

Gavana wa Lamu, Fahim Twaha ambaye pia alikuwa kwenye kikao hicho cha kujadili hali ya corona, Kaunti ya Lamu, amesema kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa, wameweka mikakati kabambe ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona.

Kulingana na Bw Twaha, kaunti imejitahidi kuweka usafi mijiji na pia kuwahamasisha wakazi kuepuka kujiweka katika makundi ambayo huenda yakawaweka kwenye hatari ya kuambukizwa corona.

Bw Twaha pia alisema Kaunti imetenga vyumba maalum kwenye baadhi ya hospitali za Lamu ili kuhudumia wagonjwa wa Covid-19

Amewataka wananchi kushirikiana na serikali ili kuona kwamba vita dhidi ya corona vinashindwa kote nchini.

“Ninawasihi wananchi kutii ushauri wa serikali. Ni vyema ubaki ndani ya nyumba yako ili kuepuka kuambukizwa maradhi hayo hatari. Isitoshe, Kaunti kwa ushirikiano na serikali ya kitaifa imeweka mikakati kabambe, ikiwemo kutenga vyumba maalum hospitalini ili kuwashughulikia wagonjwa wa Covid-19,” amesema Bw Twaha.