Habari

CORONA: Wakenya sasa waambukizana

April 6th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

WAKENYA sasa wanaambukizana virusi vya corona wao kwa wao, kwa kukiuka kanuni ambazo zimetolewa na Serikali.

Hilo lilibainika jana kwenye kikao cha maafisa wa wizara ya afya cha kuelezea kuhusu hali ya virusi hivyo nchini, ambapo idadi ya watu walioambukizwa ilifika 142, baada ya watu 16 zaidi kuthibitishwa kuambukizwa.

Kulingana na Naibu Waziri wa Afya, Dkt Mercy Mwangangi, 15 kati yao ni Wakenya, huku mmoja akiwa raia kutoka Nigeria.

Kati ya watu hao 16, tisa wanatoka katika maeneo yaliyotengwa, huku saba wakiwa miongoni mwa wale waliotangamana na watu walioambukizwa.

Maambukizi haya yanaongezeka licha ya serikali kusimamisha safari za ndege kutoka nje, ilipobainika kwamba watu wanaotoka katika nchi za kigeni ndio walikuwa katika hatari kubwa ya kusambaza virusi hivyo.

Na kutokana na hali hiyo, serikali jana ilitangaza kuanza kutekeleza hatua kali dhidi ya wahudumu wa matatu na bodaboda, ambao watakiuka kanuni zilizotolewa kwao ili kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo.

Kwenye kikao hicho, Waziri wa Uchukuzi James Macharia alisema kuwa wahudumu ambao watapatikana wakikiuka kanuni hizo wataadhibiwa vikali, ambapo leseni za vyama vyao vya matatu zutabatilishwa, huku magari yao yakitwaliwa na serikali.

Adhabu kama hiyo itatolewa kwa wahudumu wa bodaboda, kwa kuwa pikipiki zao zitatwaliwa na kushtakiwa rasmi kwa kuhatarisha afya na maisha ya watu kimakusudi.

“Kuanzia leo (Jumatatu) hali haitakuwa ya kawaida. Mhudumu yeyote wa matatu ama bodaboda ambaye atapatikana amekiuka kanuni tulizoweka atakabiliwa vikali. Tutashirikiana na Wizara ya Usalama wa Ndani kuhakikisha kuwa kanuni hizo zimezingatiwa. Polisi pia wamepewa maagizo kuhakikisha kwamba hakutakuwa na mapendeleo yoyote kwenye utekelezaji wa maagizo hayo,” akasema Bw Macharia.

Waziri alieleza sikitiko lake kwamba, kanuni hizo zilianza kukiukwa mara tu walipozitangaza.

“Tuligundua kwamba, wahudumu wa bodaboda walianza kukiuka kanuni hizo mara tu tulipozitangaza. Hii ni kwa kuwa tuliwaona wengi wao wakiwabeba hadi abiria watatu, licha ya maagizo tuliyotoa kuwataka kumbeba abiria mmoja tu. Nazo matatu nyingi zimekuwa zikiwabeba abiria wengi kupita kiasi,” akasema Bw Macharia.

Kulingana na maagizo yaliyotolewa, magari ya matatu yanapaswa kuwa na sanitaiza. Vile vile, magari hayo yanapaswa kuoshwa kila baada ya kuwabeba abiria ili kuua virusi vyovyote ambavyo huenda vitakuwepo.