Habari

CORONA: Wakenya waomba fursa wapumue

July 6th, 2020 3 min read

XINHUA Na MARY WANGARI

WAKENYA wanasubiri kwa hamu kuu hotuba ya Rais Uhuru Kenyatta leo, wakitumaini atalegeza marufuku ya kukabiliana na Covid-19 na hivyo kuwawezesha waliotenganishwa kuungana tena na familia zao, na kazi kufunguliwa.

Mfano ni Joyline Adhiambo, ambaye anatabasamu kwa matumaini akifunga zawadi anayotarajia kumpa mwanawe watakapoonana tena baada ya miezi mitatu yeye akiwa Nairobi na bintiye, 3, mashambani.

Matumaini ya Joyline ya kuonana na mtoto wake yamo kwenye imani kuwa Rais Kenyatta atalegeza marufuku ya usafiri kutoka Nairobi ambayo imekuwepo tangu Aprili 6.

Wakati marufuku hiyo ilipotangazwa mara ya kwanza, mwanawe alikuwa amesafiri mashambani naye alikuwa Nairobi, na tangu hapo hawajawahi kuonana.

“Nilikuwa ofisini Upperhill wakati Rais alipotangaza kupiga marufuku usafiri kutoka Nairobi. Nilishtuka kwani binti yangu wa miaka mitatu alikuwa mashambani na ananihitaji sana. Naomba Mungu kuwa Rais ataondoa marufuku hiyo niweze kumwona tena mtoto wangu,” asema Joyline.

“Nimekuwa nikihesabu siku zilizobaki marufuku kuisha Julai 6. Nina hamu kubwa ya kuungana tena na binti yangu,” akasema Joyline.

Yeye ni miongoni mwa maelfu ya Wakenya waliotenganishwa na familia zao, watoto na wapenzi kufuatia hatua zilizotangazwa za kukabiliana na virusi vya corona.

Martin Mureithi ni mzazi mwingine ambaye alitenganishwa na wanawe wawili, ambao marufuku hiyo ilipotangazwa walikuwa wamesafiri Mukurwe-ini, Kaunti ya Nyeri.

“Inaumiza sana kukaa miezi mitatu bila kuwaona wanangu. Naomba Uhuru aguswe aondoe marufuku ya kusafiri angaa nipate siku moja niende kuwaona,” akaambia Taifa Leo.

Hali yake ni sawa na ya Wangui Ndegwa ambaye bintiye wa miaka minne amekuwa kwao mashambani eneo la Charity, Kaunti ya Nyeri, hali naye yuko Nairobi.

Joyline anasema anatambua hatari ya kufungua nchi bila kuzingatia kanuni kikamilifu: “Najua serikali iko na wakati mgumu kuhusu suala hili, lakini nina haja kubwa kumwona binti yangu.”

MADHARA YA KIUCHUMI

“Tunajua marufuku iliyowekwa imekuwa na madhara makubwa ya kiuchumi. Lakini hatuwezi kuyaondoa kiholela,” asema Waziri Msaidizi wa Afya, Rashid Aman.

Chemutai Alonzo, 21, naye amekwama Nairobi na mawasiliano yake na wazazi ni kupitia mtandao wa Zoom, kwani walifungiwa Tanzania wanakofanya biashara tangu Kenya ilipofunga mpaka.

“Natumaini na kuomba kuwa kesho Rais atafungua mpaka wa Kenya na Tanzania niweze kuonana tena na wazazi wangu. Mawasiliano ya Zoom hayawezi kulinganishwa na kuonana ana kwa ana,” akasema Chemutai.

Mkazi Joy Wachira ambaye hufanya kazi Nairobi, alisema kwa muda wa miezi minne sasa amekwama Mombasa.

“Kazi lazima ziendelee. Kuna haja ya kaunti yetu kufunguliwa ili turudi kazini. Tutakufa njaa tukiendelea hivi,” akasema.

Erick Kiprono alisema maisha yamekuwa magumu hivyo basi Rais anapaswa kufungua nchi huku akitaka wananchi kudumisha masharti yaliowekwa.

“Tunatarajia nchi ifunguliwe kwani maisha yamekuwa magumu. Heri nchi ifunguliwe ila kwa masharti,”alisema Bw Kiprono.

Wiki iliyopita Waziri wa Usalama, Fred Matiang’i na mwenzake wa Afya, Mutahi Kagwe walisema jukumu la kuzuia maambukizi ya Covid-19 sasa limo mikononi mwa wananchi wenyewe.

Kenya imefunga baadhi ya shughuli tangu Aprili 6 wakati marufuku ya usafiri ilipotangazwa katika kaunti za kaunti zenye idadi kubwa ya maambukizi.

Hatua hiyo ilifanya watoto kutenganishwa na wazazi wao, wapenzi kushindwa kuonana huku shughuli za kiuchumi zikikwama na kuacha mamilioni katika hali mbaya kiuchumi.

Rais Kenyatta wiki iliyopita alitoa ishara ya uwezekano wa kufungua tena uchumi ikiwemo kurejewa kwa safari za ndege za humu nchini.

“Tutaanzisha safari za ndege za humu nchini na hizi ndizo tutakazotumia katika siku chache zijazo. Kwa sababu tunaondoa marufuku ambayo tumekuwa nayo baina ya kaunti ninafikiri hatua hiyo ndiyo itakayotuelekeza kwa siku ya kufungua tena safari za ndege kimataifa,” alisema Rais Kenyatta.

Huku Wakenya wakijawa na matumaini, wanafahamu vyema athari ya kulegeza mikakati hiyo bila kanuni mwafaka.

Matumaini ya Wakenya ya Rais Kenyatta kufungua tena taifa na uchumi imejiri huku visa vya Covid-19 vikizidi kuongezeka.

Kufikia jana, visa vya maambukizi Kenya vilikuwa 7886 huku watu 160 wakiwa wamefariki kutokana na gonjwa hilo na wengine 2,287 wakipona.

Hata hivyo, huku visa hivyo vikizidi kuongezeka, Wizara ya Afya imeripoti kwamba Kenya ina kiwango cha chini cha vifo ya asilimia 2.29 ikilinganishwa na jumla ya asilimia 6.7 duniani.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita, kaunti nyingi zimekuwa zikijitahidi kufikia kiwango kinachohitajika ili kuamua iwapo taifa litafunguliwa tena.

Miongoni mwa masharti hayo ni pamoja na kuwa na vituo vyenye angalau vitanda 300, mfumo wa kufanyia majaribio katika viwango vya kaunti na nafasi ya kugundua na kudhibiti visa miongoni mwa mengine.