Habari Mseto

Corona: Wanasiasa lawamani Pwani

October 20th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

BAADHI ya wakazi katika Kaunti ya Mombasa wamewalaumu viongozi wa kisiasa kwa kuchangia katika kuongezeka kwa maambukizi ya maradhi ya Covid-19.

Wakizungumza na Taifa Leo, wakazi hao walisema joto la kisiasa nchini lizimwe kwanza hadi pale janga la corona litakapoisha. Pia wamependekeza mikutano yote ya hadhara isitishwe kabisa.

Mkurugenzi wa kituo cha uvumbuzi cha SwahiliPot Hub, Mombasa, Bw Mahmood Noor, aliwalaumu wanasiasa kwa kuwa mfano mbaya, hasa wanapofanya mikutano mikubwa bila kuzingatia kanuni za kujikinga na corona.

Bw Noor alisema kuwa baadhi ya viongozi wamepuuza kuvalia barakoa na wanatangamana bila kujali, tabia ambazo wananchi wanaiga bila kujali, ndiposa idadi ya wanaoambukizwa corona inazidi kupanda kila siku.

“Shida kubwa imetokea wakati siasa imehusishwa katika vita dhidi ya janga la corona. Mwananchi wa kawaida anapomwona kiongozi wa kisiasa akifanya mikutano yenye maelfu ya watu bila kuzingatia hatua zilizowekwa kuzuia maambukizi ya corona, huenda hata nao wakapuuza,” akasema Bw Noor.

“Hatari ni kuwa maambukizi yanavyozidi kuongezeka, watu wanazidi kupuuza hatua za kujikinga na hivyo kuwaeka hatarini wale ambao wanaathiriwa pakubwa na maradhi ya Covid-19,” akasema Bw Noor huku akiwasihi wakazi wenzake wajikinge ili waweze kuwalinda wazee ambao wana uwezekano mkubwa wa kuathiriwa.

Mkazi mwingine, Bw Martin Kyalo, aliiomba serikali iache kuwabagua watu katika vita vya corona pale ambapo kuna wale ambao wanalazimishwa kufuata maagizo yaliyowekwa na Wizara ya Afya ya kujikinga dhidi ya corona, na wengine wanakosa kuyazingatia.

Jumapili, Oktoba 18, visa 685 vipya vya wagonjwa walioambukizwa virusi vya corona vilishuhudiwa kwa kipindi cha saa 24 pekee, na kufikisha idadi ya jumla ya wagonjwa walioambukizwa Covid-19 nchini kuwa 621,976 tangu kisa cha kwanza kutangazwa mnamo Machi mwaka huu.

Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe, alisema kuwa asilimia ya maambukizi imeongezeka hadi 12 kutoka kwa asilimia nne iliyokuwepo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza ufunguzi wa uchumi taratibu.

Bw Kagwe alitaja kaunti za Nairobi, Mombasa na Nakuru kama maeneo ambapo maambukizi yameongezeka sana, huku akiwaomba wakazi waendelee kujikinga.