Habari Mseto

CORONA: Watu 100 kutengwa kwa mwezi mzima

April 4th, 2020 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WATU zaidi ya 100 waliotengwa kwa siku 14 kama tahadhari ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona humu nchini, wamepata pigo baada ya kulazimishwa kusalia karantini kwa mwezi mmoja.

Kati ya watu 2,050 waliokuwa wametengwa kwa lazima na serikali, 1,886 wameruhusiwa kurejea nyumbani baada ya kumaliza siku 14 karantini na kuthibitishwa kuwa hawana virusi vya corona.

Jumla ya watu 184 wamesalia katika karantini na kundi hili ambalo baadhi yao watatengwa kwa muda wa mwezi mmoja kwa kukiuka masharti ya kuwataka kutokaribiana, kwa mujibu wa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe.

Hatua hiyo ya serikali inamaanisha kuwa mtu mmoja akipatikana na virusi vya corona, wenzake waliotengwa kwenye jengo hilo wanaongezewa siku 14 zaidi.

“Imebainika kuwa baadhi ya watu waliotengwa katika vituo mbalimbali, wamepuuza kanuni zilizowekwa na wizara ya Afya kuhusu kutokaribiana na usafi na wamekuwa wakitangamana tu kiholela. Tabia hiyo inawatia katika hatari ya kuambukizana virusi vya corona,” akasema Bw Kagwe.

Kulingana na serikali, ni vigumu kuwaruhusu kuondoka kwani wanaweza kuwa wameambukizwa virusi siku chache zilizopita baada ya kupimwa damu.

Kwa kawaida, watu waliotengwa wanagharimia chakula na malazi katika maeneo wanayoishi.

Jana, waziri Kagwe alisema kuwa serikali itawasaidia kulipia sehemu ya gharama ya siku za ziada watakazokuwa karantini.

Ripoti zinaonyesha kuwa baadhi ya watu walio kwenye karantini wamekuwa wakinywa pombe na hata kula pamoja.

Hayo yanajiri huku idadi ya watu waliothibitishwa kuwa na virusi vya corona ikiongezeka kutoka watu 122 hadi 126. Hiyo ni wa Afya baada ya watu wengine wanne, jana kuthibitishwa kuwa na virusi vya corona.

“Katika muda wa saa 24 zilizopita tumepima zaidi ya watu 372 na kati yao wanne walipatikana na virusi vya corona. Watatu kati ya waliopatikana na virusi walikuwa Wakenya na mmoja raia wa Pakistani,” akasema waziri Kagwe.

Waziri alisema kuwa serikali inafuatilia watu 672 wanaosadikiwa kutangamana na watu ambao wamethibitishwa kuwa na virusi vya corona.

Alisema serikali inaendelea na mipango ya kuwatengenezea wahudumu wa afya vifaa na mavazi ya kuwazuia kuambukizwa virusi vya corona.