Habari Mseto

Corona: Watu 40 kushiriki majaribio ya chanjo Kenya

September 19th, 2020 1 min read

Na MISHI GONGO

WATU 40 wanatarajiwa kuanza kufanyiwa majaribio ya chanjo dhidi ya virusi vya corona nchini hivi karibuni.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Kenya (KEMRI), Dkt Kombe Yeri alisema jana kuwa chanjo hiyo inayofahamika kama ChAdox1 nCoV-19 itajaribiwa kwa watu hao wa kujitolea, kabla ya kufanyiwa watu zaidi.

“Kikundi cha majaribio ya KEMRI kimepokea idhini kutoka kwa kamati ya Ukaguzi wa Maadili ya Sayansi ya KEMRI, Bodi ya Dawa na Sumu, Tume ya Kitaifa ya Teknolojia ya Sayansi na Ubunifu (NACOSTI) na kwa sasa inasubiri idhini kutoka kwa mamlaka zinazoidhinisha matumizi ya chanjo,” akaeleza.

KEMRI inaongoza majaribio nchini Kenya kupitia ushirikiano na Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza.

Majaribio yalikuwa yamefika katika awamu ya tatu Uingereza lakini yakasitishwa kwa muda wakati kulipotokea madhara ya kiafya kwa mtu mmoja kabla ya kurejelewa tena.

‘Kufikia sasa watu wa kujitolea 8,000 wamepokea chanjo hiyo nchini Uingereza, Brazil na Afrika Kusini,’ akasema Dkt Yeri.Dkt Yeri aliongeza kuwa, maoni ya umma yatahusishwa kabla majaribio hayo kuanza nchini.

Mwenyekiti wa kamati ya afya bungeni, Bi Sabina Chege alisifu taasisi hiyo kwa juhudi zake.Urusi tayari imeidhinisha chanjo ambayo mataifa kadhaa yameagiza.