Habari Mseto

CORONA: Waumini wagomea ibada

March 16th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WAUMINI wa makanisa mengi nchini Jumapili walikosa kuhudhuria ibada wakihofia kuambukizwa virusi vya corona.

Hata hivyo, makanisa mengi yaliweka tahadhari kali kukabili uenezaji wa ugonjwa huo, baada ya serikali kuthibitisha kisa cha kwanza cha virusi hivyo wiki iliyopita.

Katika Kaunti ya Kisumu, uchunguzi wa ‘Taifa Leo’ ulibaini makanisa mengi yaliweka dawa ya kuua viini ili kutumiwa na washirika wake.

Katika kanisa la Christ is the Answer Ministries (CITAM) Kisumu, mashemasi watatu waliwekwa katika lango kuu la kuingia kanisa hilo, huku kila mmoja akiwekea washirika dawa hiyo kujipaka mikononi. . Hali ilikuwa hivyo katika kanisa Katoliki la St Joseph’s.

“Ili kuzingatia kanuni zilizotolewa na Wizara ya Afya, tunamruhusu mshirika kuingia baada tu ya kujipaka dawa hiyo,” akasema mwenyekiti wa Baraza la Parokia, Bw Barrack Okumu.

Katika Kaunti ya Kisii, ni washirika wachache tu ambao walifika katika kanisa Katoliki la Kisii Cathedral.

Kaasisi Lukas Ong’esa alichukua jukumu la kuwafunza washirika kuhusu tahadhari wanazopaswa kuchukua ili kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.

“Lazima kila mmoja wetu achukue tahadhari, kwa kunawa mikono kwa sabuni na maji kama njia ya kukabili makali ya virusi hivyo,” akasema.

Katika Kaunti ya Homa Bay, Wakristo wengi walifuata agizo la serikali kuzingatia usafi.

Makanisa mengi yaliamua kutumia maji na sabuni kuwaosha washirika wake ili kuwazuia kuambukizwa.

Baadhi ya washirika hata hivyo waliamua kubeba dawa hizo, ambapo waliwagawia wale ambao hawakuwa nazo.

Washirika katika kanisa la Kianglikana (ACK) la Christ the Healer mjini Homa Bay waliamua kutumia maji na sabuni.

Katika Kaunti ya Vihiga, uchunguzi ulibaini kwamba ibada ziliendea katika makanisa mengi bila uzingatiaji wa kanuni hizo.

Kinyume na maeneo mengine, washirika wengi walifika makanisani, huku wakisalimiana na kukaa karibu bila hofu zozote.

Hata hivyo, viongozi mbalimbali wakiwemo Seneta George Khaniri, wabunge Beatrice Adagala, Charles Gimose (Hamisi) na Godfrey Osotsi walitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuwa waangalifu.

Katika Kaunti ya Migori, kanisa la Kiadventista (SDA) lilifutilia mbali mikutano yote ya ibada kutokana na hofu ya virusi hivyo.

Katika Kaunti ya Mombasa, washirika wengi walionekana kuepuka kusalimiana na kukumbatiana.

Makanisa mengi pia yaliweka dawa za kuzuia viini hivyo, ambapo washirika waliwekewa kwa mikono kujipaka kabla ya kuruhusiwa kuingia makanisani.

Katika Kaunti ya Nakuru ibada ziliendelea kama kawaida.Waumini walimimikika katika makanisa mbalimbali kuhudhuria ibaada zao kama ilivyo ada.

Hata hivyo, kulikuwepo na taratibu ambazo walitakiwa kufuata kama vile kujipaka dawa ya kuua viini kwanza.

Wakati wa kupokea sakramenti takatifu, waumini walihitajika kutumia mikono yao ya kushoto na kisha kutia midomoni kwa kutumia mikono ya kulia.

Ripoti za: Ondari Ogega, George Odiwuor, Benson Ayienda, Derrick Luvega, Shaban Makokha, Siago Cece, Phyllis Musasia na Waikwa Maina