Habari

Corona yaangusha shujaa

July 11th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HALI ya majonzi imekumba sekta ya afya na wahudumu walio kwenye mstari wa mbele kupambana na virusi vya corona, baada ya daktari kuangamizwa na virusi hivyo.

Dkt Doreen Adisa Lugaliki, 38, alithibitishwa kufariki usiku wa kuamkia jana baada ya kukimbizwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa matibabu.

Daktari huyo wa uzazi, aliambukizwa virusi vya corona akiwa kazini. Alianza kuugua Jumatatu na kukimbizwa katika hospitali ya Aga Khan kwa matibabu.

Alikuwa akihudumu katika Hospitali ya Nairobi South. Alikuwa ni mama wa watoto pacha wenye umri ya miaka 13.

Akitoa taarifa ya kila siku kuhusu hali ya janga la corona nchini, Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe alithibitisha kuwa marehemu ni kati ya watu wanane waliofariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 ndani ya saa 24 zilizopita.

Idadi ya waliofariki kwa Covid-19 nchini sasa imefika watu 181.

Dkt Lugaliki ni mhudumu wa kwanza wa Afya kufariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19, tangu kisa cha kwanza cha ugonjwa kiliporipotiwa nchini mnamo Machi 13.

“Dkt Lugaliki alipata virusi hivyo wakati alikuwa anajikamamua kuokoa maisha ya wengine. Tunasikitika kuwa tumempoteza huyo mwenzetu ambaye ni miongoni mwa mashujaa wetu katika vita hivi vya kupambana na Covid-19,” Bw Kagwe alisema katika kaunti ya Kilifi.

Waliohudhuria kikao hicho walitakikana kutulia kwa dakika moja kwa heshima ya Dkt Lugaliki.

Wengi waliotuma risala zao za rambirambi walihimiza Wakenya watambue kuwa, wanapopuuza maagizo wanayopewa kuhusu udhibiti wa virusi vya corona, wanaweka pia maisha ya madaktari hatarini ilhali ndio wanajeshi wao katika vita hivi.

“Heshima yetu kuu kwa Doreen sharti iwe ni kudumisha nidhamu kwa kufuatia kanuni za kuzuia maambukizi ya ugonjwa huu,” akasema Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Jana, idadi ya wagonjwa wa Covid-19 ilifika 9,448 baada ya watu 473 kupatikana wameambukizwa virusi vya corona.

Jumla ya wagonjwa 76 walipona na kuruhusiwa kwenda nyumbani, hivyo kufikisha 2,733 idadi ya wale ambao wamepona kufikia jana.

Kupitia kwa Chama cha Wahudumu wa Matibabu na Madaktari wa Meno (KMPDU), madaktari walisema sasa Serikali inafaa kutilia uzito hitaji la kuwahakikisha usalama wao wakati huu wa janga la corona.

“Tunasisitiza na kuikumbusha Serikali na hospitali zote za kibinafsi kwamba, usalama wetu sio wa kufanyiwa mjadala. Tumempoteza mtaalamu, mama, rafiki na mwenzetu kazini,” chama hicho kilisema kwenye taarifa.

Mkurugenzi wa Afya, Dkt Patrick Amoth alisema kifo cha daktari huyo ni dhihirisho tosha kuwa janga hilo linashambulia bila kubagua.

Dkt Amoth alisema kuwa kufikia sasa jumla ya wahudumu wa afya 292 wameambukizwa virusi vya corona; ambapo 160 kati yao ni wa jinsia ya kike na 132 ni wanaume.

Seneta wa Siaya James Orengo alimwomboleza daktari huyo kama shujaa ambaye alijizatiti kuhakikisha raia wenzake wako salama.

Marehemu alipata mafunzo yake katika Chuo Kikuu cha Nairobi katika ngazi ya shahada ya kwanza na ile ya uzamili.