Habari

Corona yaendelea kushika wakubwa

March 28th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

VIRUSI vya corona vinavyoendelea kutikisa dunia, vimedhihirisha havina ubaguzi wa tabaka la mtu baada ya idadi ya viongozi wa kimataifa na watu mashuhuri wanaoambukizwa kuendelea kuongezeka.

Ijumaa, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ndiye aliyeingia kwenye orodha ya watu mashuhuri ulimwenguni ambao wamethibitishwa kuambukizwa, na ikabidi ajitenge.

Awali Jumatano, Mwanamfalme wa Uingereza Prince Charles, ambaye anatarajiwa kurithi ufalme iwapo mamake Malkia Elizabeth ataondoka, pia alitangazwa kuambukizwa virusi vya corona.

Nchini Amerika, Seneta wa Chama cha Republican anayesimamia jimbo la Kentucky, Rand Paul alipatikana na ugonjwa huo pia

Kufikia sasa, kiongozi mwingine wa mamlaka ya juu aliyeambukizwa corona ni Makamu wa Rais wa Iran, Massoumeh Ebtekar.

Baada ya kutangaza kuwa aliambukizwa Machi 11, maafisa kadhaa wakuu wa serikali hiyo pia walipimwa wakapatikana waliambukizwa.

Nchini Burkina Faso, maafisa kadhaa wa serikali wakiwemo mawaziri Oumarou Idani (madini), Stanislas Ouaro (elimu) na Simeon Sawadogo (usalama wa nchi) walitangazwa kuugua corona.

Vilevile, Waziri wa Mashauri ya Kigeni nchini humo Alpha Barry pia aliambukizwa.

Kando na viongozi wa kisiasa, idadi kubwa ya watu mashuhuri katika nyanja mbalimbali wakiwemo wanamuziki, wanariadha na wachezaji mashuhuri wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

Mwigizaji mashuhuri wa Hollywood Tom Hanks na mkewe Rita Wilson walitangaza mnamo Machi 11 kuwa waliambukizwa ugonjwa huo.

Mwingine ni Idris Elba kutoka Uingereza, ambaye alitangaza hali yake kupitia kwa video aliyopeperusha mitandaoni mnamo Machi 16.

Katika nchi jirani ya Tanzania, mwimbaji mashuhuri Mwana FA na meneja wa mwimbaji Diamond Platnumz, Sallam Sharaff walitangaza kwamba walipatikana kuambukizwa corona.

Waimbaji waliothibitishwa kufariki kutokana na corona ni Manu Dibango aliyeaga mnamo Machi 25.

Mwingine ni mwimbaji mashuhuri wa mtindo wa Soukous kutoka Congo, Aurlus Mabele ambaye alifariki wiki iliyopita.

Katika ulingo wa spoti, meneja wa Arsenal Mikel Arteta alitangaza mnamo Machi 12 kwamba aliambukizwa.

Katika siku hiyo hiyo, winga wa klabu ya Chelsea, Callum Hudson-Odoi pia alitangaza hali yake ni sawa na hiyo.

Wachezaji wengine wa kandanda ambao wanauguza virusi hivyo ni Blaise Matudui wa klabu ya Juventus na mwenzake Daniele Rugani.

Katika timu ya Deportivo Alaves ya Uhispania, iliripotiwa wachezaji 15 walithibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.

Kuna idadi kubwa ya wachezaji mpira wa vikapu ambao wamethibitisha kuugua ugonjwa huo kufikia sasa.

Kufikia jana jioni watu wapatao elfu 560 walikuwa wamethibitishwa kuambukizwa virusi hivyo na zaidi ya elfu 25 kuaga.

Tiba ya virusi vya corona haijapatikana ingawa kuna aina mbalimbali za dawa ambazo zinatumiwa kwa sasa kutibu wagonjwa. Wengi wamepona katika nchi mbalimbali ikiwemo Kenya ambapo mtu mmoja alithibitishwa kupona wiki hii.

Hapo Ijumaa, Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, alisema idadi ya Wakenya waliothibitishwa kuambukizwa ingali 31 huku mmoja akifariki Jumatano na mwingine akipona.

Haya yanajiri huku Amerika ikichukua uongozi wa visa vingi zaidi vya maambukizi duniani na kushinda China, ambayo ndiyo chimbuko la maradhi hayo yaliyozuka Desemba 2019.

Jumla ya watu elfu 86 walikuwa wameambukizwa Amerika kufikia jana jioni ikifuatwa na China kwa visa elfu 81 na Italia elfu 80.

Kwa upande wa vifo, Italia ilikuwa ingali mbele kwa kupoteza watu zaidi ya elfu 8 na kufuatwa na Uhispania yenye zaidi ya elfu 4.

Jumla ya mataifa 199 kote duniani yametangaza maambukizi ya virusi hivyo ambavyo vinasambaa kwa haraka.

Mataifa mengi ikiwemo Kenya yameweka kafyu katika juhudi za kupunguza watu kukusanyika.